Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi ameeleza kufurahishwa kwa kutengewa siku yake maalum katika mcihezo wao wa leo Jumatano dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Uongozi wa Yanga juzi ulitangaza kuwa kwa kutambua mchango wa kocha huyo, mchezo huo wa Dodoma utakuwa maalum kwake.
Yanga imekuwa ikifanya hivyo kwa wachezaji wake katika baadhi ya mechi lakini pia hivi karibuni katika mechi na mahasimu wao Simba waliyoshinda kwa mabao 2-1 ilikabidhiwa kwa Wazee wa Jangwani.
Gamondi alisema kwake ni faraja lakini anaona kama si yeye anayestahili hadhi hiyo kwani wapo wengi nyuma yake waliofanikisha mafanikio ya Yanga msimu huu.
Alisema kwamba ndio ambao wanastahili heshima na hadhi hiyo kutokana na mchango wao mkubwa wakiwemo wasaidizi wake wa benchi la ufundi.
“Kila wakati ni vizuri kutambulika na klabu, mashabiki juu ya uwepo wako lakini hii si ya kwangu binafsi, nyuma kuna kundi la watu waliofanikisha haya kuanzia watu wa benchi la ufundi, watu wanaofanya idara ya afya, ofisini, hawa wote wanafanya haya yawezekane na kuleta mafanikio.
“Labda ukizungumzia mimi pengine ninasimama upande wa maamuzi tu au kuleta mawazo na vitu vya namna hiyo lakini bila hawa wengine hakuna kinachofanyika.
“Nafikiri hii inawahusu wao, na hii si ya kwangu binafsi ila inawahusu wote waliofanya kazi ndani ya klabu hii na kuleta furaha kwa namna moja ama nyingine,” alisema Gamondi.
Kocha huyo raia wa Argentina aliyetua Yanga msimu huu akitokea Ittihad Tanger ya Morocco kurithi mikoba ya Nassredine Nabi aliyetimkia FAR Rabat, msimu huu amefanikiwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu NBC, kuipeleka Yanga robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuifikisha kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho CRDB ambapo wataumana na Azam FC.
Soka Gamondi afurahi kupewa siku Yanga
Gamondi afurahi kupewa siku Yanga
Read also