Liverpool, England
Mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah ameonesha dalili zote za kubaki Liverpool baada ya kuahidi kuendelea kuipigania mataji timu hiyo kwa nguvu zote licha ya kuondoka kwa kocha Jurgen Klopp.
Salah anaingia katika mwaka wake wa mwisho wa mkataba wake wa sasa na hadi sasa hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa baina ya klabu na mchezaji huyo ili kumuongezea mkataba zaidi ya muda uliobaki.
Majira ya kiangazi msimu uliopita, Liverpool ilikataa ofa ya Pauni milioni 150 ili kumuuza Salah katika klabu ya Al Ittihad ya Saudi Arabia ingawa kwa sasa zipo habari kwamba klabu hiyo huenda ikaamsha upya mpango huo.
Mara baada ya Klopp kuaga rasmi Liverpool na kocha mpya, Arne Slot kutangazwa rasmi, majaliwa ya Salah katika klabu hiyo yalianza kujadiliwa na kukawa na hofu kwamba huenda naye akaondoka.
Kupitia mitandao ya kijamii, Salah hata hivyo ameupinga mpango wowote wa kuondoka baada ya kusema kwamba atakuwa na Liverpool msimu ujao na azma yake ni kuipa mafanikio timu hiyo.
“Tunajua kwamba mataji ndio kitu muhimu na tutafanya kila kinachowezekana kuliwezesha hilo msimu ujao, mashabiki wetu wana haki katika hilo na tutapambana hakuna mfano,” alisema Salah.
Salah, 31, pia alimpongeza kocha anayeondoka Klopp ambaye hivi karibuni walitibuana katika mechi dhidi ya West Ham kwa kinachodhaniwa kuwa alichukia kuwekwa benchi na kocha huyo.
“Ni jambo kubwa kubeba mataji na kupata uzoefu nawe katika miaka saba iliyopita, nakutakia heri kwa mambo yako yajayo, natumaini tutakutana tena,” alisema Salah katika posti yake kwenye mitandao ya kijamii iliyoambatana na picha yake akiwa na Klopp.