Na mwandishi wetu
Hatimaye meneja habari na mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe amesema bado hawajafanikiwa kumuongezea mkataba kiungo wao mshambuliaji, Stephane Aziz Ki.
Kamwe pia alisema kwamba kuwa jukumu la mchezaji huyo kuendelea kukipiga Jangwani lipo mikononi mwa mashabiki na wanachama wao.
Akizungumzia umuhimu wa mashabiki na wanachama wa Yanga hii leo Jumatano jijini Dar es Salaam, Kamwe alisema mashabiki na wanachama Yanga wana wajibu wa kulipa ada ya usajili wa uanachama ili kumudu baadhi ya mambo ya klabu ikiwemo kuendelea kuwa na wachezaji mahiri kama Aziz Ki.
“Mashabiki wengi wananipigia simu kuhusu Aziz Ki. Sasa niwaambie kama wewe ni shabiki wa Yanga na hulipi kadi ya uanachama basi ujue wataondoka wachezaji wengi tu.
“Ili Aziz Ki abaki lazima klabu iwe na hela na hela zinatoka kwetu sisi. Tumewapa fursa ya kulipa ada kupitia mataw ya NBC. Je wachezaji wanabaki vipi ikiwa wewe hulipi ada?
“Hili nimesema nilizungumze hapahapa na niliweke wazi kabisa, mambo mnayoyasikia yakizungumzwa ndiyo maana hata sisi hatutaki kuyaongelea, kwa sababu tunajua hamna timu hapa Tanzania Aziz Ki anaweza kwenda kucheza zaidi ya Yanga, ila tunajua watu wanaomtaka Aziz wako vizuri kweli kipesa.
“Hiyo ni kweli sina hata haja ya kuanza kufanya propaganda, ningekuwa mtu wa propaganda ningewaambia kwamba tayari Aziz yupo lakini hayupo, bado na ni jukumu langu mimi na wewe mwanachama wa Yanga kuhakikisha tunajisajili na Aziz anabakia, huo ndiyo uhalisia wenyewe hakuna siasa hapa, tusipeane moyo wakati uhalisia tunaukimbia,” alisema Kamwe.
Hivi karibuni kumeibuka tetesi lukuki juu ya nyota huyo raia wa Burkinafaso kuwaniwa na vigogo wa Afrika wakiwemo Kaizer Chiefs, Orlando Pirates na Mamelodi Sundowns za Afrika Kusini pamoja na Al Ahly na Pyramids za Misri.
Aziz ambaye amejiunga na Yanga msimu wa 2022-23 akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast ameonesha kiwango kikubwa mpaka sasa akiwa amefunga mabao 15 msimu huu kabla ya mechi yao ya leo dhidi ya Dodoma Jiji akiwa amezidiwa bao moja na kinara Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam aliyefunga mara 16 mpaka sasa.