Na mwandishi wetu
Mshambuliaji hatari wa Tanzania wa timu ya wanawake ya Al Nassr ya Saudi Arabia, Clara Luvanga amekutana kwa mara ya kwanza na nyota wa klabu hiyo kwa timu ya wanaume, Cristiano Ronaldo.
Clara ambaye amekuwa tishio tangu atue Nassr msimu huu akitokea Dux Logrono ya Hispania, ameelezea furaha aliyokuwa nayo baada ya kukutana na mchezaji huyo bora duniani aliyewahi kutamba na timu za Man United, Real Madrid na nyinginezo.
Katika kuonesha furaha aliyokuwa nayo, Clara ameweka picha kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii akiwa ameshikana mkono na nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ureno huku nyuma yao kukiwa na nembo kubwa ya Al Nassr.
“likuwa ndoto kukutana naye na kupiga picha naye, hatimaye ndoto yangu imetimia. Nina furaha sana kukutana naye” ameandika Clara kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.
Kama ilivyo kwa Ronaldo, 39 ambaye ni kinara wa mabao wa timu hiyo na ligi ya wanaume ya Saudi Arabia akiwa na mabao 33, Clara pia ni miongoni mwa washambuliaji tishio wa timu hiyo akiwa amepachika mabao 11.
Clara hata hivyo anashika nafasi ya nne kwenye orodha ya wafungaji wa ligi ya wanawake lakini ni wa pili kwa timu yake, akizidiwa na Mualgeria, Lina Boussaha aliyefunga mabao 12.
Wakati Al Nassr ya wanaume ikiwa ni ya pili dhidi ya wababe Al Hilal, Clara ambaye makabrasha yake yanaonesha amezaliwa mwaka 2005, ameiongoza Al Nassr ya wanawake kutwaa ubingwa wa nchi hiyo.