London, England
Wachezaji Marcus Rashford na Jordan Henderson wameachwa katika kikosi cha awali cha England kinachojiandaa kwa fainali za michuano ya Kombe la Ulaya (Euro 2024) nchini Ujerumani.
Rashford, 26, ambaye ni mshambuliaji wa Man United, amekuwa na wakati mgumu msimu huu akiwa hadi sasa amefunga mabao saba tu na kutoa asisti mbili katika mechi 33 za ligi alizocheza.
Kwa upande wa England msimu huu Rashford ameichezea timu hiyo mechi saba kabla ya kuachwa katika kikosi cha timu hiyo kilichocheza na Ubelgiji takriban miezi miwili iliyopita.
Rashford mara baada ya kuachwa katika timu hiyo aliamua kutumia mitandao ya kijamii na kutuma ujumbe wa kumtakia kila la heri kocha wa England, Gareth Southgate na vijana wake katika fainali za Euro 2024.
Kwa upande wa Henderson mchezaji huyo wa zamani wa Liverpool, alitimkia Saudi Arabia majira ya kiangazi mwaka jana na kujiunga na klabu ya Al-Ettifaq lakini Januari mwaka huu aliondoka katika timu hiyo na kujiunga na Ajax ya Uholanzi.
Akiwa Al-Ettifaq, Southgate aliwahi kumuita katika kikosi cha England kwenye mechi dhidi ya Ausralia iliyopigwa kwenye dimba la Wembley Oktoba mwaka jana.
Mechi hiyo hata hivyo ilikuwa ngumu kwa Henderson ambaye alijikuta akizomewa na mashabiki jambo lililomkera Southgate na kusema kwamba zomea zomea dhidi ya mchezaji huyo haina maana.
Henderson ambaye Southgate amesema kumuacha katika kikosi chake ni uamuzi mgumu, pia aliitwa katika mechi za kirafiki za England dhidi ya Brazil na Ubelgiji lakini hakucheza.
Juni 7 itakuwa siku ya mwisho kwa Southgate kutangaza kikosi cha mwisho ambapo atalazimika kupunguza wachezaji saba katika timu ambayo imepanfwa Kundi C na itacheza mechi ya kwanza Juni 16 dhidi ya Serbia na kufuatiwa na mechi nyingine mbili dhidi ya Denmark na Slovenia.
Kikosi kamili cha England kinaundwa na makipa: Aaron Ramsdale (Arsenal), James Trafford (Burnley), Dean Henderson (Crystal Palace) na Jordan Pickford wa Everton.
Mabeki: Jarrad Branthwaite (Everton), Lewis Dunk (Brighton), Joe Gomez (Liverpool), Marc Guehi (Crystal Palace), Ezri Konsa (Aston Villa) na Harry Maguire (Man United).
Mabeki wengine ni Jarell Quansah (Liverpool), Luke Shaw (Man United), John Stones (Man City), Kieran Trippier (Newcastle) na Kyle Walker (Man City)
Viungo ni Trent Alexander-Arnold (Liverpool), Conor Gallagher (Chelsea), Curtis Jones (Liverpool), Kobbie Mainoo (Man United), Declan Rice (Arsenal) na Adam Wharton (Crystal Palace).
Washambuliaji: Jude Bellingham (Real Madrid), Jarrod Bowen (West Ham), Eberechi Eze (Crystal Palace), Phil Foden (Man City), Jack Grealish (Man City), Anthony Gordon (Newcastle), Harry Kane (Bayern Munich), James Maddison (Tottenham), Cole Palmer (Chelsea), Bukayo Saka (Arsenal), Ivan Toney (Brentford) na Ollie Watkins (Aston Villa).
Kimataifa Rashford, Henderson waachwa England
Rashford, Henderson waachwa England
Read also