Manchester, England
Kocha wa Man City, Pep Guardiola ambaye jana Jumapili aliweka rekodi ya kubeba taji la Ligi Kuu England, (EPL) kwa mara ya nne mfululizo na timu hiyo huenda msimu ujao ukawa wa mwisho kwake na klabu hiyo kwa alichodai kuwa amechoka.
Pep ana mkataba unaofikia ukomo mwaka 2025 ambao ana nia ya kuutumikia lakini baada ya hapo alisema anadhani hatosaini mkataba mwingine mpya na yuko karibu kuondoka kuliko kuendelea kubaki.
“Tumezungumza na klabu na mtazamo wangu ni kwamba nataka kubaki wakati huu, nitaendelea kuwa hapa msimu ujao na katika kipindi cha msimu huo tutazungumza lakini baada ya miaka minane au tisa…, tutaona,” alisema Pep.
Pep, 53 hadi sasa ana rekodi ya kubeba mataji 15 mbalimbali kwa kipindi cha miaka minane akiwa na Man City na Mei 25 anaweza kutwaa taji la 16 kama timu yake itatoka na ushindi dhidi ya Man United katika mechi ya fainali ya Kombe la FA.
Kocha huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich amekiri kuwa amechoka na kwa sasa anapoanza mapumziko anahitaji mazingira tofauti na mapya ya kumhamasisha kabla ya kuanza msimu mpya wa 2024-25 mwezi Agosti.
“Nina mkataba kwa hiyo bado niko hapa, kuna mambo kidogo yameanza kunichosha lakini kuna ambayo nayapenda na tuko hapa kushinda mechi, tunasubir mambo yawe mazuri na wachezaji wapya,” alisema Pep.
Kuhusu kushinda mataji manne ya EPL mfululizo, Pep alisema kwamba awali alianza kufikiria kuwa hakuna aliyefanya hivyo na kwa nini asijaribu na sasa anaona amekamilisha kazi lakini hapo hapo anajikuta akijiuliza nini kinafuata.