Liverpool, England
Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp jana Jumapili aliwaaga mashabiki wa timu hiyo huku akiliimba jina la mrithi wake Arne Slot mbele ya mashabiki hao katika uwanja wa nyumbani wa Anfield.
Klopp amekuwa na Liverpool kwa kipindi cha miaka minane na nusu, alihitimisha majukumu yake kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wolverhampton katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu England (EPL) msimu wa 2023-24.
Mabao hayo yaliyofungwa katika kipindi cha kwanza na Alexis Mac Allister na Jarell Quansah pia yalihitimisha ushindi wa 305 kwa kocha huyo katika mechi 491 alizoiongoza Liverpool hadi sasa.
Slot aliyekuwa kocha wa timu ya Feyenoord ya Uholanzi alithibitishwa Ijumaa iliyopita kuwa ndiye atakayebeba mikoba ya Klopp ambaye alitangaza mapema kuwa hatoendelea na timu hiyo baada ya msimu huu.
“Kocha mpya, nataka muliimbe jina lake,” Klopp alisema kuwaambia mashabiki kabla ya kuendelea, kuwaimbisha kwa wimbo wenye ujumbe wa kumtaka Slot abebe majukumu akiwa kamili msimu mpya utakapoanza huku akimtaka ajiamini na asiache kufanya hivyo.
“Naona watu wengi wanalia, na mimi pia lakini mabadiliko ni jambo zuri, kama unakwenda na hulka sahihi na kila kitu kitakuwa sawa,” alisema Klopp.
Klopp alisema kuna wakati alikuwa katika kipindi kibaya lakini anashukuru Mungu si leo (Jumapili) badala yake anashukuru kwa yote yaliyotokea kwa kuwa unapokuwa vizuri unasahau hata yale yaliyobora na kuona ni ya kawaida.
Chini ya Klopp, Liverpool imefanikiwa kubeba mataji yote makubwa isipokuwa taji la Europa Ligi, na katika msimu wa 2019-20 walibeba taji la EPL na kufuta ukame wa miaka 30 tangu wabebe taji hilo mara ya mwisho.