London, England
Baada ya Man City kubeba taji la Ligi Kuu England (EPL), kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amewakikishia mashabiki wa timu hiyo kwamba mwishowe timu yao italibeba taji hilo.
Arteta pia ametaka timu hiyo kutoridhika kwa kushika nafasi ya pili na kuhakikisha wanalibeba baada ya kulikosa katika hatua ya mwisho kwa misimu miwili mfululizo.
Arsenal jana Jumapili iliifunga Everton mabao 2-1 ushindi ambao haukuiwezesha timu hiyo kubeba taji la EPL baada ya Man City iliyokuwa ikiongoza ligi hiyo kwa pointi mbili nayo kutoka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya West Ham.
Baada ya mechi hiyo iliyopigwa kwenye dimba la Emirates, Arteta alizungumza na mashabiki na kuwataka kutokata tamaa na kuendelea kuiunga mkono timu na kubwa ni kutoridhika baada ya timu hiyo kushika nafasi ya pili.
“Huu sasa ni wakati wa kupumzika, na kutafakari na tafadhali endeleeni kuiunga mkono timu, kuipa hamasa, msiridhike kwa sababu tunataka mafanikio zaidi ya haya na tunakwenda kuyapata,” alisema Arteta.
Alipoulizwa ni kwa nini anajiamini namna hiyo, Arteta alisema kwamba kama watafanya wanachotakiwa kukifanya na kuyakaribia mafnikio mwishowe watabeba taji.
“Ni lini? Sijui lakini kama tutaendelea kupambana na kuwa karibu na taji mwisho wa siku tutafanikiwa kulibeba,” alisema Arteta.
Arsenal imemaliza ligi ikiwa na pointi 89 ambazo ni nyingi kwa rekodi za ligi hiyo lakini imezidiwa pointi mbili na Man City ambao pia wameweka rekod ya kubeba taji hilo kwa mara ya nne mfululizo.