Na mwandishi wetu, Arusha
Hatimaye Yanga imefuzu kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho CRDB baada ya kuilaza Ihefu FC bao 1-0 katika mechi iliyopigwa leo Jumapili kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
Kwa ushindi huo Yanga sasa itaumana na Azam FC katika mechi ya fainali itakayopigwa Juni 2 mjini Manyara, Azam imefuzu hatua hiyo baada ya kuilaza Coastal Union 3-0 katika nusu fainali nyingine iliyopigwa kwenye dimba la CCM Kirumba mjini Mwanza.
Bao pekee lililoipa ushindi Yanga leo lilifungwa na Stephanie Aziz Ki akiutumia mpira ulioanzia kwa Khalid Aucho ambaye alimuunganishia Pacome Zouzoua aliyepiga krosi ya chinichini na Ki kuunganisha moja kwa moja hadi wavuni.
Haikuwa rahisi kwa Yanga kupata bao hilo kwani mechi hiyo ililazimika kuchezwa kwa dakika 120 baada ya timu hizo kushindwa kufungana katika dakika 90 za kawaida na ndipo Yanga walipopata bao lao dakika ya 10 katika dakika 30 za nyongeza.
Kocha wa Ihefu, Mecky Maxime alisema mchezo ulikuwa mzuri na hana sababu yoyote ya kuwalaumu wachezaji wake kwa matokeo hayo kwani kufanya hivyo ni kuwakosea.
Kwa upande wake kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema kwamba mechi ilikuwa ngumu na kuwapongeza Ihefu kwa namna walivyokaba vizuri lakini pia aliwapongeza wachezaji wake kwa kuonesha ukomavu wa kisoka.
Katika hatua nyingine Gamondi pia alilalamikia hali ya uwanja kwa alichosema kwamba haukuwa mzuri kwa timu zote.
Naye kiungo wa Yanga, Mudathir Yahya alitangazwa kuwa nyota wa mchezo huo na kukabidhiwa hundi ya Shs 500,000 ambazo zilitolewa na wadhamini wa michuano hiyo, Benki ya CRDB.
Mudathir alimshukuru Mungu kwa kupata tuzo hiyo na kuwapongeza wachezaji wenzake kwa ushirikiano pamoja na benchi la ufundi la timu yake.
Soka Ni Yanga, Azam fainali CRDB
Ni Yanga, Azam fainali CRDB
Read also