Na mwandishi wetu
Kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Hemed Morocco amesema anaamini kikosi chake kitacheza kwa mabadiliko makubwa kuelekea mechi yao ya marejeano itakayopigwa kesho Jumapili dhidi ya Sudan katika Uwanja wa King Fahad nchini Saudi Arabia.
Stars ambayo ina kikosi chenye wachezaji vijana wengi kuelekea michezo hiyo miwili dhidi ya Sudan ambapo katika mchezo wa kwanza uliopigwa juzi Jumatano, Stars ilipoteza kwa mabao 2-1.
Akizungumza leo Jumamosi moja kwa moja na GreenSports kutoka Saudia, Morocco alieleza kuwa wamefanyia kazi mapungufu mengi waliyoyaona kwenye mechi ya kwanza.
Alisema kwamba vijana wake wanaonekana kuelewa na kubadilika kila kukicha hivyo ni imani yake wataendeleza walichojifunza kuelekea mechi hiyo ya kesho.
“Tumerudi kwenye uwanja wa mazoezi kujaribu kurekebisha kile ambacho kilionekana kwenye mechi ya mwanzo, tulianza vibaya tukaruhusu mabao yale mawili lakini tulivyorudi kipindi cha pili tulikua wazuri zaidi.
“Kesho itakuwa mwendelezo wa pale tulipoishia kipindi cha pili maana ingawa tulipoteza lakini naamini marekebisho tuliyoyafanya tunaweza kucheza vizuri kesho na kupata matokeo,” alisema Morocco.
Morocco pia alisema kuwa anafurahi kuona kambi ya timu hiyo kiujumla inakwenda vizuri kwa namna wachezaji wanavyoelewa mapema na kukifanya kwa ufasaha kile wanachoelekezana na kuuona mwelekeo mzuri zaidi kwa siku za usoni kwa timu hiyo.