Na mwandishi wetu
Makocha Charles Boniface Mkwasa (pichani) na Abdallah Kibadeni wamefurahishwa na kulipongeza Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kwa kurejesha michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu Kombe la Kagame.
Cecafa kupitia taarifa yao iliyowekwa juzi na mtendaji wao mkuu, John Gecheo ilitangaza kurejesha michuano hiyo inayotarajia kuanza kutimua vumbi Julai 20 hadi Agosti 4 mwaka huu huku Tanzania Bara ikiwa mwenyeji.
Michuano hiyo inarejea kwa mara ya kwanza baada ya mara ya mwisho kufanyika mwaka 2021 nchini Tanzania na Express ya Uganda kuibuka mabingwa.
“Ni mashindano yatakayosaidia sana timu zinazoshiriki michuano mikubwa Afrika kujiandaa, itakuwa ni sawa na maandalizi yao kuelekea michuno.mingine mbalimbali mikubwa Afrika na hata ligi kuu yenyewe,” alisema Mkwasa, kocha na nahodha wa zamani wa Yanga.
Naye kocha wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Kibadeni aliunga mkono kurejeshwa michuano hiyo na kueleza kwamba pia itakuwa na faida nyingine za kuwasaidia wachezaji wa Stars katika timu zao.
Alisema michuano hiyo pia itazisaidia klabu kupata michuano mingi itakayozidi kuwaimarisha na kuwaweka kiushindani stahiki muda wote kutokana na upinzani tofauti watakaokuwa wakikutana nao.
Michuano hiyo itajumuisha timu shiriki 16 ambapo zipo zitakazotoka miongoni mwa nchi wanachama wa Cecafa huku nyingine zikitoka kwa nchi zitakazopata mwaliko.
Wanachama wa Cecafa ni Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, Sudan, Eritrea, Zanzibar, Sudan Kusini, Somalia na Djibouti.
Soka Mkwasa, Kibadeni wafurahia Cecafa
Mkwasa, Kibadeni wafurahia Cecafa
Read also