Manchester, England
Kiungo wa Man City, Phil Foden ametangazwa kuwa mchezaji bora wa msimu wa Ligi Kuu England (EPL) ikiwa ni siku moja kabla ya timu yake kucheza mechi ya mwisho iliyobeba hatma ya taji la ligi hiyo msimu huu.
Hayo ni mafanikio ya pili kwa kiungo huyo wa England mwenye umri wa miaka 23 ambaye mapema mwezi uliopita alipigiwa kura na kuibuka mshindi wa tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka wa Chama cha Waandishi wa Soka.
Hadi sasa Foden anajivunia kuifungia Man City mabao 17 msimu huu huku akibebwa na asisti nane katika EPL huku kesho Jumapili timu yake ikicheza mechi ya mwisho ya msimu huu dhidi ya West Ham.
“Kushinda tuzo hii ni mafanikio ambayo kwa hakika najivunia, ligi kuu inafahamika kuwa ni ligi iliyo bora duniani na ni jambo la kujivunia kuteuliwa mbele ya wachezaji wengi bora ambao wote wameufurahia msimu mzuri katika klabu zao,” alisema Foden.
Kwa Man City ni Erling Haaland pekee aliyefunga mabao mengi (27) na kumzidi Foden ambaye pia anaisubiri kwa hamu hiyo kesho akisubiri kuona timu yake ikipata ushindi na kubeba taji la EPL kwa mara ya nne mfululizo.
“Kiujumla nimekuwa mwenye furaha mno kwa namna ambavyo nimekuwa nikicheza msimu huu na najivunia kwa jinsi nilivyoweza kutoa mchango kwa mabao na asisiti katika kipindi chote cha msimu,” alisema Foden.
Foden pia alitumia nafasi hiyo kuwashukuku maofisa wote wa klabu ya Man City, makocha na wachezaji wenzake kwa sababu bila ya wao haingewezekana na pia aliwashukuru wote waliompigia kura hadi kushinda tuzo hiyo yenye maana kubwa kwake.