Na mwandishi wetu
Yanga imeamua kuweka kando sherehe za ubingwa na kuwekeza katika kusaka ushindi wakitambua kuwa na kibarua kigumu cha nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Ihefu FC.
Meneja habari na mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe amesema kulingana na rekodi baina yao kuelekea mchezo huo utakaopigwa Mei 19, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha utakuwa mgumu.
Kamwe alisema kwa hiyo wanalazimika kuungana na kusahau kwa muda shangwe za ubingwa wao wa Ligi Kuu NBC waliotwaa hivi karibuni ili kukamilisha kazi iliyo mbele yao.
“Ni mchezo mgumu kweli kweli niwaambie mashabiki na wanachama wa Yanga, wawe tayari sababu Ihefu tulipata matokeo mazuri kwenye mechi ya marudiano katika ligi tukashinda mabao 5-0 lakini mchezo wa kwanza tulipoteza dhidi yao na ni timu chache msimu huu tumegawana nazo pointi kwenye ligi.
“Hivyo tunapoenda kwenye Kombe la Shirikisho tunapaswa kwenda kikubwa, kwenda na akili zote, twende na utayari wote kuhakikisha tunakwenda kupambana, Yanga yetu inakwenda fainali japo tunafahamu shauku ya Wanayanga wanachotaka kusikia ni maandalizi ya sherehe za ubingwa.
“Lakini niwaambie vitu hivi vinaenda sambamba, kwamba lazima kwa sasa tuungane twende sambamba kuhakikisha tunaenda fainali na naamini Yanga tukiungana tunalifanya hili,” alisema Kamwe.
Kabla ya mchezo huo, utatangulia mchezo wa nusu fainali ya kwanza Mei 18, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza baina ya Azam FC dhidi ya Wagosi Wakaya, Coastal Union.