Na mwandishi wetu
Baraza la Michezo Tanzania (BMT) limesema kuwa Tuzo za BMT zitafanyika Juni 9 mwaka huu huku vipengele viwili vikiongezwa katika tuzo hizo.
Mwenyekiti wa kamati ya Tuzo BMT, Mtumbuka Mtambo, amesema vipengele vilivyoongezeka ni tuzo za mwaka 2023 zitakazotolewa ni vipengele vya tuzo ya kocha bora wa mwaka na mwamuzi bora wa mwaka.
Alisema kwamba lengo la kuongeza vipengele hivyo ni katika kuhakikisha wadau wote wa sekta za michezo wanatambulika na kuthaminiwa.
“Mabadiliko mengine ni uwepo wa tuzo za jumla mwaka huu na si za mchezo mmoja mmoja, mabadiliko haya yanalenga kuleta ushindani na ufanisi ikiwa ni pamoja na kuleta usawa wa uthamani wa michezo yote, kadhalika mabadiliko haya yanaongeza thamani ya tuzo hizi kiujumla,” alisema Mtambo.
Naye, mwenyekiti wa BMT, Leodegar Tenga (pichani juu) kuelekea msimu wa pili mfululizo wa utolewaji wa tuzo hizo, alisema kwa kifupi kuwa ni muhimu kuwepo kwa tuzo hizo kwani zinachagiza maendeleo ya michezo katika kila nyanja kuanzia kukuza viwango vya ushindani mpaka uwekezaji.
“Faida za tuzo ni kubwa sana lakini kwa maneno machache ni kuhamasisha, kuchagiza maendeleo ya michezo kwa maana ya kukuza kiwango, kuna kuchagiza uwekezaji kwenye michezo maana bila uwekezaji hali ni ngumu, haiwezekani hata kidogo, nchi zote zilizofanya vizuri zimewekeza,” alisema Tenga.