Manchester, England
Mshambuliaji mkongwe Man United, Wayne Rooney amesema timu hiyo inahitaji mabadiliko makubwa katika usajili ambapo ameshauri timu mpya iundwe kupitia nahodha Bruno Fernandes.
Man United ipo nafasi ya nane kwenye Ligi Kuu England (EPL) na Mei 25 itaikabili Man City katika fainali ya Kombe la FA, mechi ambayo inatakiwa ishinde ili kujihakikishia nafasi ya kucheza michuano ya klabu Ulaya.
Fernandes amekuwa mchezaji pekee ambaye ameonesha kiwango kilichovutia wengi na hadi sasa ndiye anayeongoza kwa mabao timu hiyo akiwa amezifumania nyavu mara 10 na kutoa asisti saba na kuwazidi wenzake wote.
“Unalazimika kuijenga timu kupitia Bruno, ni mchezaji pekee wa kiwango, ana tabia ya upambanaji, nafikiri inatakiwa kuwaacha wachezaji wachanga pamoja na Bruno, nafikiri kunatakiwa kufanywa mabadiliko makubwa, iwe hivyo,” alisema Rooney.
Rooney mmoja wafungaji bora waliowahi kuichezea Man United hata hivyo alitahadharisha kwamba jambo hilo si la kufanywa kwa mwaka mmoja badala yake linahitaji miaka kadhaa.
“Kushindana katika ligi hii unahitaji wachezaji walio bora na msininukuu vibaya, wachezaji hawa ni wazuri na ni wachezaji wa ligi kuu lakini ili kushindana na Manchester City, Liverpool, Arsenal unahitaji wachezaji walio bora,” alisema Rooney.
Akimzungumzia Marcus Rashford, Rooney alisema, “Sote tunamfahamu Marcus ana sifa za kucheza katika ligi ya juu, najaribu kufikiria kwamba huenda huu ni wakati wake wa kwenda kucheza soka sehemu nyingine, japo sina uhakika na hilo.”
Rooney alisema kwamba Rashford anatakiwa kulitafakari jambo hilo, kujiuliza maswali na hatimaye arudi katika uchezaji ambao wote tunajua anaweza kuwa.