Riyadh, Saudi Arabia
Winga wa Al Nassr ya Saudi Arabia, Cristiano Ronaldo ametajwa na jarida maarufu la Forbes kuwa ndiye mwanamichezo anayelipwa fedha nyingi zaidi duniani, akishika nafasi hiyo kwa mara ya nne mfululizo.
Kwa mujibu wa jarida hilo maarufu duniani mwanamichezo anayeshika nafasi ya pili ni mcheza golfu, Jon Rahm wa Hispania ambaye amejipatia mafanikio hayo baada ya kuhamia Saudi Arabia.
Baada ya kujiunga na Al Nassr, Ronaldo, 39, alitangazwa kuwa mwanamichezo anayelipwa fedha nyingi zaidi ambapo pato lake kwa ujumla limefikia Dola 260 milioni, kiwango ambacho ni cha juu zaidi kwa mwanasoka.
Mapato ya Ronaldo yanayotokana na ushiriki wake katika soka yanamuingizia Dola 200 milioni wakati yale ya nje ya soka yanayotokana na udhamini wa makampuni mbalimbali yanafikia Dola 60 milioni yakichangiwa na mamilioni ya wafuasi katika mitandao ya kijamii hasa Instagram.
Jumatano iliyopita, Ronaldo alinukuliwa akisema angependa kuendelea kucheza soka licha ya ukweli kwamba umri wake unakaribia miaka 40, umri ambao alitakiwa afikirie kustaafu au awe tayari amestaafu.
Na kwa upande wa Rahm, hivi karibuni aliishtua dunia ya wanamichezo baada ya kutangazwa kuwa pato lake linaweza kufikia kiasi cha Dola 300 milioni.
Kwa sasa kilicho wazi ni kwamba pato la nyota huyo wa golfu limefikia Dola 218 milioni na hivyo kuungana na Ronaldo kuwa wanamichezo pekee ambao pato lao limezidi Dola 200 milioni.
Nafasi ya tatu katika orodha hiyo ya Forbes imekwenda kwa mshambuliaji wa zamani wa Barcelona na PSG, Lionel Messi ambaye kwa sasa anaichezea Inter Miami ya Marekani, pato lake linafikia Dola 135 milioni.
Wa nne katika orodha hiyo ni nyota wa kikapu wa Los Angeles Lakers, LeBron James ambaye pato lake limefikia Dola 128.2 milioni, James huenda akastaafu mpira wa kikapu hivi karibuni.
Anayeshika nafasi ya tano na pato lake kwenye mabano ni nyota mwingine wa kikapu, Giannis Antetokounmpo wa Milwaukee Bucks (Dola 111 milioni).
Nahodha wa timu ya taifa ya Ufaransa na mshambuliaji wa PSG anayetajwa kuwa mbioni kujiunga na Real Madrid, Kylian Mbappé yuko nafasi ya sita akiwa na pato linalofikia Dola 110 milioni.
Wengine wanaofuata ni wanasoka Neymar wa Brazil anayeichezea Al Hilal ya Saudi Arabia (Dola 108 milioni) na Karim Benzema ambaye pia anakipiga Saudi Arabia (Dola 106 milioni).
Kimataifa Ronaldo aongoza kwa mkwanja duniani
Ronaldo aongoza kwa mkwanja duniani
Read also