Na mwandishi wetu
Kaimu kocha mkuu Simba, Juma Mgunda amesema wanaihitaji nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu NBC kutokana na umuhimu wao wa kuwakilisha nchi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
Mgunda ameyazungumza hayo muda mchache kabla ya kuelekea Dodoma kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Dodoma Jiji utakaochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Ijumaa hii kuanzia saa 10 jioni.
“Ukiwa unajua matokeo ya mpira yapo ya aina ngapi basi inakuwa haisumbui kidogo, tunajua kabisa tunakwenda kushindana na washindani wa mpira wenzetu.
“Basi yale yalikuwa matokeo ya mpira (1-1 dhidi ya Kagera Sugar), tumejifunza baada ya matokeo yale nini cha kwenda kufanya katika mchezo wetu wa Dodoma sababu matokeo ya Dodoma kwetu ni muhimu sana.
“Muhimu sababu moja ya malengo ya timu kwa kuwa bingwa ameshapatikana, nafasi ya pili ni muhimu kwa ajili ya uwakilishi wa nchi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa, kwa hiyo tunalijua hilo, tunalifahamu na tunalitambua.
“Kwa hiyo maandalizi yote ya kuendelea kushindana katika mechi hizi nne zilizobaki ni kuhakikisha tunafanya vizuri na mwisho wa yote kukipata tulichokusudia kukipata,” alifafanua Mgunda.
Simba ipo nafasi ya tatu kwa pointi 57 baada ya mechi 26 ikichuana na Azam FC inayoshika nafasi ya pili kwa pointi 60 baada ya kushuka dimbani mara 27.
Yanga ikiwa tayari imetangaza ubingwa baada ya kufikisha pointi 71 ilizovuna kwenye mechi 27, ikisaliwa na michezo mitatu mkononi.
Simba ikimalizana na Dodoma, itamalizia mechi zake tatu ikiwa nyumbani dhidi ya Geita Gold, KMC na JKT Tanzania wakati Azam itapepetana na JKT Tanzania ugenini, kisha na Kagera ikiwa nyumbani kabla ya kwenda ugenini kufunga dimba na Geita Gold.