Na mwandishi wetu
Meneja habari na mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amewapongeza mahasimu wao Yanga kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu NBC msimu huu ikiwa ni msimu wa tatu mfululizo wanafanya hivyo.
Akizungumza Jumanne hii, Ally alisema kwamba anawapongeza Yanga kwa kazi nzuri waliyoifanya na hatimaye kufanikiwa kubeba taji hilo.
Ally hata hivyo alisema wanawapongeza lakini wakifahamu wao pia wana mengi ya kujifunza, kujikosoa na kurekebisha kutokana na kutotwaa taji hilo kwa msimu wa tatu mfululizo wakishuhudia likitua Yanga.
“Tuwapongeze kwa kazi nzuri waliyoifanya na hatimaye kupata ubingwa, wameibuka namba moja na hatuna budi kuwapongeza kwa kazi kubwa waliyoifanya.
“Na sisi kama Simba tunayo mengi ya kujilaumu, tunayo megi ya kujifunza ya kujikosoa na ya kurekebisha na inapaswa kukaa chini na kuona wapi tunakosea na huu ni msimu wa tatu tunamaliza bila ubingwa,” alisema Ally.
“Kwa hiyo hii imemalizika kwa maana ya ubingwa lakini inafungua nafasi nyingine ya kupigania nafasi ya thamani iliyobaki kwenye ligi yetu nayo ni nafasi ya pili, sasa hivi tumelingana alama na Azam na tuna kila sababu ya kufanya vizuri ili tuchukue nafasi ya pili katika ligi ya msimu huu,” alisema Ally.
Mpaka Jumatatu, Yanga inatawazwa bingwa baada ya kuifunga Mtibwa Sugar mabao 3-1, ilifikisha pointi 71 ambazo hazitafikiwa na timu nyingine huku Azam FC ikiwa na pointi 60 katika nafasi ya pili baada ya mechi 27 na Simba inashika nafasi ya tatu kwa pointi 57 baada ya mechi 26.