Na mwandishi wetu
Yanga hatimaye imefanikiwa kulibeba taji la Ligi Kuu NBC msimu wa 2023-24 baada ya kuichapa Mtibwa Sugara mabao 3-1 katika mechi iliyopigwa Jumatatu hii kwenye dimba la Manungu, Turiani mjini Morogoro.
Ushindi huo unaifanya Yanga iwe imelibeba taji la ligi ikiwa na mechi tatu mkononi na inalibeba kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kufanya hivyo katika msimu wa 2021-22, 2022-23 na sasa 2023-24.
Matokeo ya ushindi dhidi ya Mtibwa yameifanya Yanga ifikishe jumla ya pointi 71 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote inayoshiriki ligi hiyo zikiwa zimebaki mechi mbili hadi tatu kabla ya msimu wa ligi kufikia tamati.
Mtibwa ambayo ina hali mbaya kwenye ligi ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 32 mfungaji akiwa ni Charles Ilamfya na kuonekana kama bao hilo lingeweza kuichelewesha Yanga katika mbio zake za kulibeba taji hilo.
Yanga ilianza kujibu mapigo dakika ya 63 ikisawazisha kupitia Kennedy Musonda kabla ya kupata bao la pili ambalo Nassir Kombo alijifunga katika dakika ya 67 wakati bao la ushindi la Yanga lilifungwa na Clement Mzize dakika ya 81.
Mafanikio hayo pia yanaifanya Yanga iwe imekata tiketi ya moja kwa moja kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu ujao huku ikiziacha Azam FC na Simba zikichuana kuwania nafasi ya pili ambayo kwa sasa inashikiliwa na Azam.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezwa Jumatatu, Tanzania Prisons ikiwa nyumbani ililala kwa bao 1-0 mbele ya Ihefu FC wakati Singinda FG ikiwa ugenini ililazimisha sare ya bao 1-1 mbele ya JKT Tanzania.
Soka Yanga yabeba taji Ligi Kuu NBC
Yanga yabeba taji Ligi Kuu NBC
Read also