Paris, Ufaransa
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amesema ana matumaini kuwa mshambuliaji Kylian Mbappe wa PSG ataiwakilisha Ufaransa kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris, baadaye mwaka huu.
Macron aliyasema hayo Jumamosi ikiwa ni siku moja baada ya Mbappe kuthibitisha kuwa ataachana na PSG huku akihusishwa kwa kiasi kikubwa na mipango ya kujiunga na Real Madrid
“Sina maoni yoyote maalum ya kuyasema zaidi ya ukweli kwamba tunaitegemea Real Madrid kuwa itamruhusu Kylian awemo kwenye Michezo ya Olimpiki, aiwakilishe timu ya Ufaransa,” alisema Rais Macron.
Kabla ya kutoa kauli hiyo, Macron pia alinukuliwa mwezi uliopita akisema kwamba anadhani klabu za Ulaya zinahitaji kuwaruhusu wachezaji kwenye Olimpiki ili michezo iwe yenye hadhi.
Mwezi Machi mwaka huu, Mbappe naye alinukuliwa kabla ya mechi ya Ufaransa na Ujerumani akisema angependa kuwamo kwenye Michezo ya Olimpiki lakini uamuzi wa jambo hilo si wake peke yake.
Wakati huo huo, kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti alikataa kuhusishwa na ujio wa Mbappe katika klabu hiyo kuhusu siku ambayo wanatarajia kumpokea mchezaji huyo.
Kuhusu hoja ya Rais wa Ufaransa, Ancelotti pia alisema hawezi kutoa maoni yoyote kuhusu kauli ya kiongozi huyo kwa kuwa hana haki ya kufanya hivyo.
Kimataifa Rais Macron amtaka Mbappe kwenye Olimpiki
Rais Macron amtaka Mbappe kwenye Olimpiki
Read also