London, England
Kocha wa Arsenal Mikel Arteta kwa sasa anajiandaa kuivaa Man United katika mechi muhimu ingawa akili ya kocha huyo kwa sasa inawaza kulibeba taji la Ligi Kuu England (EPL) msimu huu.
“Ubongo wangu wakati wote unanipeleka mahali ambapo tunabeba taji la ligi kuu, hapo ndipo ulipo ubongo wangu kwa wakati huu,” alisema Arteta.
Arsenal kwa sasa inashika usukani wa EPL ikiwa imeizidi Man City inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi moja na wanaweza kutupwa nafasi ya pili kama Man City watashinda mechi yao ya kesho Jummosi dhidi ya Fulham.
Arsenal nayo inaweza kurejea kileleni iwapo itatoka na ushindi katika mechi yake ya Jumapili dhidi ya Man United, timu ambayo kwa sasa mambo yake si mazuri kwenye ligi hiyo.
Arteta hata hivyo alionekana mwenye kuyajua mazingira hayo aliposema kwamba hali ipo wazi na wanalazimika kuwa makini na wanachokifanya ili kuwa katika nafasi nzuri na hicho ndicho kitu wanachokifanya kwa sasa.
Baada ya mechi dhidi ya Man United itakayopigwa kwenye dimba la Old Trafford, Arsenal itakuwa mwenyeji wa Everton katika mechi yao ya mwisho itakayopigwa Mei 19 wakati Man City itakuwa na mechi Jumanne dhidi ya Tottenham kabla ya kumaliza ligi kwa mechi dhidi ya West Ham.
“Tuko katika safari ya kujaribu kuwakamata, ni jambo zuri kwa wakati wote inapotokea kuna mtu anayekupa changamoto ya kwenda mbali zaidi na zaidi,” alisema Arteta.
Arteta alisema kwamba historia ya Man City imekuwa ni ya kubeba mataji na wamekuwa wapinzani wa kipekee kwa miaka takriban 15 iliyopita na Arsenal wanachotaka ni kubadili hali hiyo.