Madrid, Hispania
Mshambuliaji wa Real Madrid, Vinícius Júnior amepuuza habari za kwamba ana uwezo wa kushinda tuzo ya Ballon d’Or badala yake amesema anachoangalia kwa sasa ni vipi ataiwezesha timu yake kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya 15.
Vinicius Jr, usiku wa Jumatano alitangazwa kuwa nyota wa mchezo wakati Real Madrid ikiumana na Bayern Munich katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
“Kila mtu anaizungumzia Ballon d’Or lakini kwa upande wangu nimetulia, ninachotaka ni kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara nyingine na timu hii,” alisema Vinicius.
Alisema anaamini anaweza kufanya mambo makubwa msimu huu na baada ya hapo aende na timu ya taifa ya Brazil kwenye Copa America na kwamba kwa wakati wote yeye huwa anaifikiria timu kwanza na baada ya hapo ndipo anajifikiria yeye binafsi.
“Tumeweza kuifikisha timu bora katika fainali nyingine, tuna mastaa 25 kwa pamoja tumefanya bidii ili kufanikisha azma yetu ya kwenda London kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na kushinda taji la La Liga, tumeshashinda La Liga na tunakwenda London,” alisema Vini.
Katika siku za hivi karibuni Vinícius ambaye ndio kwanza ana miaka 23 amekuwa akitajwa kuwa na nafasi kubwa ya kubeba tuzo ya Ballon d’Or ambayo kwa sasa inashikiliwa na Lionel Messi.
Januari mwaka huu Vinicius alipambwa mno baada ya kufunga mabao matatu peke yake (hat trick) wakati Real Madrid ikiilaza Barcelona katika fainali ya Spanish Super Cup na mabao yake 13 yamechangia kwa kiasi kikubwa kwa timu hiyo kubeba taji la La Liga.