Madrid, Hispania
Kocha wa Bayern Munich, Thomas Tuchel amesema kitendo cha mwamuzi kusimamisha mchezo kabla ya timu yake kufunga bao la kusawazisha katika mechi ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid ni mfano wa usaliti.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumatano usiku kwenye dimba la Bernabeu, Bayern walikuwa mbele kwa bao 1-0 hadi dakika ya 88 baada ya Joselu aliyeingia kipindi cha pili kufunga bao la kwanza na kuongeza la pili katika dakika tatu.
Wakati Bayern ikiwa nyuma kwa mabao 2-1 katika dakika za nyongeza, Matthijs de Ligt aliifungia Bayern bao na kudhani kuwa alisawazisha lakini mshika kibendera tayari aliinua kidendera kuashiria kwamba mfungaji alikuwa ameotea.
Mabeki wa Real Madrid, walisimama kabla ya De Ligt kuujaza mpira wavuni na baadaye marudio ya kwenye televisheni yalionesha kuwa uamuzi wa awali usingekuwa wa mchezaji kuotea na hilo lingeweza kufanyiwa mapitio ya VAR.
Hata hivyo kwa kuwa mchezo ulishasimamishwa, VAR haikuweza kutumiwa jambo ambalo Tuchel amelitaja kuwa ni uamuzi mbaya mno na ambao pia ni kinyume na taratibu.
“Kumekuwa na uamuzi wa hovyo kutoka kwa mshika kibendera na mwamuzi, mwisho wa yote tunaona kama ni kusalitiwa,” alisema Tuchel.
“Mshika kibendera alisema samahani lakini hilo halisaidii kitu, kuinua kibendera katika kipindi kama hicho, mwamuzi aliona tulikuwa tunaupata mpira na kuupiga golini, ni ngumu kukubali lakini hivyo ndivyo mambo yalivyo,” alisema Tuchel.
Baadaye Tuchel alisema kwamba mwamuzi Szymon Marciniak ambaye pia ndiye aliyechezesha mechi ya fainali ya Kombe la Dunia 2022 pia aliomba msamaha lakini kwa Tuchel jambo hilo pia haliwezi kusaidia kitu.
Kwa ushindi huo, Real sasa inasubiri kuumana na Borussia Dortmund katika mechi ya fainali ambayo itapigwa Juni Mosi mwaka huu kwenye dimba la Wembley.