Na mwandishi wetu
Simba haijakata tamaa katika kulisaka taji la Ligi Kuu NBC baada ya kuifanyia maangamizi Azam FC ikiichapa mabao 3-0 katika mechi iliyopigwa Alhamisi hii jioni kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo ingawa bado yanaiacha Simba katika nafasi ya tatu lakini yameibua hofu kwa Azam kuwa inaweza ikaipoteza nafasi ya pili wakati Yanga nayo isipokuwa makini inaweza kujikuta ikishindwa kulitetea taji la Ligi Kuu NBC msimu huu.
Kwa ushindi huo Simba sasa imefikisha pointi 56 ikiwa imezidiwa pointi moja na Azam yenye pointi 57 ingawa Simba ina faida ya mechi moja ikiwa imecheza mechi 25 wakati Azam tayari imecheza mechi 26.
Simba hata hivyo bado ina kazi ngumu ya kuiondoa Yanga kileleni kwani Yanga katika mechi zake 26 Yanga ina pointi 68 hivyo Simba hata ikishinda mechi tano zilizobaki bado itatakiwa kuombea Yanga iteleze ili kuweza kulibeba taji la Ligi Kuu NBC msimu huu.
Mabao ya Simba katika mechi na Azam yalipatikana kuanzia dakika ya 63 mfungaji akiwa ni Sadio Kanoute wakati bao la pili likifungwa dakika ya 77 na Fabrice Ngoma kabla David Kameta hajakamilisha hesabu ya mabao kwa kuandika bao la tatu dakika moja kabla ya kutimia dakika 90.
Soka Simba yaiangamiza Azam
Simba yaiangamiza Azam
Read also