Na mwandishi wetu
Uongozi wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) umesimamishwa ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili ikiwemo ya matumizi mabaya ya madaraka, ukiukaji wa Katiba ya Kamisheni hiyo na mgongano wa maslahi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa (pichani), hatua hiyo imechukuliwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt Damas Ndumbaro baada ya kikao cha jana Jumatano kilichofanyika jijini Dodoma.
Imeelezwa zaidi kuwa kufuatia uamuzi huo, Waziri Ndumbaro ameunda kamati ya mpito ya kuongoza kamisheni hiyo ambayo itaongozwa na Mwenyekiti Emmanuel Salehe na viongozi wengine wakiwa ni Alex Galinoma (Makamu Mwenyekiti), Joseph Mpuya (Katibu Mkuu) na wajumbe ni Patrick Nyembela, Shaffi Dauda na Irene Mwasanga.
Ndumbaro pia ameunda kamati ya kufanya uchunguzi kwa kamisheni iliyosimamishwa kuhusu tuhuma hizo mbalimbali zilizoibuliwa na wanachama wao.
Kamati hiyo itafanya kazi kwa muda wa mwezi mmoja kuanzia Mei 8 mwaka huu ikiongozwa na mwenyekiti Christopher Kamugisha akiwa na katibu Ingridy Kimario, wajumbe ni Mariam Aziz Faki na Sophia Alponary.
Ndumbaro pia amewataka wadau wa michezo kote nchini kufuata sheria, kanuni na miongozo iliyopo kwenye vyama na mashirikisho ya michezo ili azma ya serikali ya kukuza na kuendeleza
michezo nchini itimie.