Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Kagera Sugar, Obrey Chirwa amesema anaamini kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ni mchezaji mzuri zaidi ya Stephanie Aziz Ki wa Yanga, isipokuwa Fei anashushwa chini kutokana na uhalisia wa nchi yake, Tanzania.
Chirwa ambaye anatokea nchini Zambia amezungumza hayo na kufafanua kwamba amekuwa akiiona hali ya wachezaji wa Kitanzania kutokukubalika nchini na badala yake wadau huvutiwa zaidi na wanaotoka nje.
Alisema hali hiyo huwakuta wachezaji hao hata kama wana viwango vya kawaida lakini yeye binafsi anaamini ni nchi yenye wachezaji wenye viwango vikubwa mno tofauti na watu wanavyodhani.
“Ukiachana na Diarra (Djigui wa Yanga), nilishakutana na makipa wengi wakali wa Tanzania kama Aishi Manula au Beno Kakolanya, wale wana hatari ujue ila shida ni kwamba Watanzania mnawadharau wenzenu, mnapenda vipya lakini Watanzania wana uwezo mkubwa kushinda ‘maforena’,” alisema Chirwa ambaye timu yake ilifungwa bao 1-0 na Yanga.

“Mnaona mabeki wa kati wa Yanga, wale ni Watanzania lakini watu wanawadharau wanawaona wa kawaida tu. Mfano viungo yaani ina wale kina Mudathir (Yahya), Feisal ni hatari wale siwezi kusema sana lakini mambo yanaelweka.
“Hata Fei na Aziz, Fei yupo juu lakini sababu ni Mtanzania watu wanamchukulia poa mbele ya wageni,” alisema Chirwa ambaye pia aliwahi kukipiga Yanga.
Chirwa aliyewahi pia kukipiga Nogoom FC ya nchini Misri ameongelea ushindani wa Fei na Aziz Ki kwa kuwa pia wanachuana msimu huu msimu huu.

Wachezaji hao ambao walikuwa na ushirikiano mzuri wakati wakiwa Yanga kabla ya Fei kutimkia Azam kwa sasa wamefungana kileleni kwa mabao 15 huku Aziz akiwa juu kwa kutoa pasi za mabao nane na Fei akitoa pasi saba mpaka sasa (kabla ya mechi ya Simba na Azam).