Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa PSG, Kylian Mbappe amesema kushindwa kwa timu yake kufuzu hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kulala kwa bao 1-0 mbele ya Borussia Dortmund, sababu ni kupoteza nafasi zikiwamo alizopoteza yeye.
PSG ikiwa nyumbani katika jiji la Paris, jana Jumanne ililala kwa bao 1-0 na hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 2-0 baada ya kulala kwa bao 1-0 katika mechi ya nusu fainali ya kwanza.
Kwa matokeo hayo, Dortmund sasa inasubiri kucheza mechi ya fainali kwenye dimba la Wembley na mshindi wa mechi nyingine ya nusu fainali kati ya Real Madrid na Bayern Munich leo Jumatano.
Akizungumza baada ya matokeo hayo, Mbappe alisema kwamba katika mechi hiyo alijaribu kadri alivyoweza kuisaidia timu yake lakini hapo hapo alikiri kushindwa kufanya hivyo kiasi cha kutosha.
“Tunapozungumzia kuwa sahihi katika eneo la boksi, nafikiri mimi hapo ndiye mlengwa, mimi ni mtu ambaye ni lazima nifunge mabao na niwe makini, mambo yanapokuwa mazuri nabeba sifa zote na inapokuwa tofauti nabeba lawama, hilo si tatizo,” alisema Mbappe.
Akifafanua zaidi Mbappe alisema mtu wa kwanza ambaye ilikuwa lazima afunge ni yeye na kwamba kilichojitokeza ndivyo maisha yalivyo na sasa ni lazima yeye na wenzake waangalie mbele.
Mchezaji huyo ambaye anahusishwa na mipango ya kujiunga na Real Madrid alisema kwamba PSG si kwamba haikuwa na bahati bali haikuwa katika ubora kiasi cha kutosha.
PSG ambao walifanya mashambulizi kadhaa yakiwamo mashuti yaliyogonga mwamba, jambo ambalo Mbappe alisema linaonesha jinsi ambavyo hawakuwa vizuri na kwa upande wa Dortmund alisema hana uhakika kama timu hiyo ilikuwa bora zaidi yao.
“Sipendi kuzungumzia suala la kutokuwa na bahati, unapokuwa vizuri mashuti hayawezi kugonga mwamba, yanaingia nyavuni, leo (jana) hatukuwa vizuri sisi washambuliaji,” alisema Mbappe.
Bao lililoibeba Dortmund lilipatikana mapema kipindi cha pili mfungaji akiwa ni Mats Hummels na baada ya hapo timu hiyo ilifanya kazi nzuri kumdhibiti Mbappe ambaye huenda hiyo ikawa mechi yake ya mwisho ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na jezi ya PSG.

Mbappe hata hivyo alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu kujiunga na Real Madrid aliishia kukunja uso na kuondoka.
Naye kocha wa PSG, Luis Enrique aliwapongeza Dortmund kwa ushindi na kusema kwamba kilichoikuta timu yake kinasikitisha hasa kwa namna ambavyo walicheza vizuri na kufanya mashambulizi ya kutosha.
“Inasikitisha unapopoteza mchezo hasa kwa namna hii, tumegonga mwamba wa goli mara sita, tumepiga mashuti 31 lakini hatukuweza kufunga goli, inaonekana kama ni jambo gumu kuamini,” alisema Enrique.
Dortmund wakifanikiwa kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu watakuwa wanafanya hivyo kwa mara ya kwanza tangu kufanya hivyo mara ya mwisho mwaka 1997.