London, England
Kocha wa Man United, Erik ten Hag amesema kwamba timu yake imecheza chini ya kiwango na hatimaye kukutana na kiipigo cha mabao 4-0 mbele ya Crystal Palace jana Jumatatu katika mechi ya Ligi Kuu England (EPL).
Matokeo hayo yanazidi kuiweka pagumu timu hiyo na kuhatarisha nafasi yake ya kuwamo kwenye michuano ya klabu barani Ulaya kwa msimu ujao.
Man United kwa sasa inashika nafasi ya nane kwenye EPL na hivyo kwa wakati huu haimo kwenye nafasi ya timu zitakazocheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Nafasi pekee ya Man United inayoipigania Ulaya ni kwenye Europa Ligi kupitia Kombe la FA ambapo inajiandaa kuumana na bingwa mtetezi Man City kwenye mechi ya fainali.
Man United inakabiliwa na kipindi kigumu ikiwamo janga la majeruhi ambapo wachezaji 10 wa kikosi cha kwanza ni majeruhi lakini Ten Hag alishikilia msimamo wa timu kucheza chini ya kiwango na hivyo kukutana na kipigo hicho kikubwa cha msimu.
“Ni jambo lililo wazi, hiki ni kiwango cha chini, hatukukabiliana nao kwa namna tulivyotaka na hatukuwa vizuri kwa kiasi kikubwa,” alisema Ten Hag.
Kocha huyo hata hivyo pamoja na kulaumu kiwango cha timu yake, alikiri ukweli kwamba ana tatizo la majeruhi katika kiwango ambacho amedai hakuwahi kukutana nacho katika kazi yake ya ukocha.