Na mwandishi wetu
Yanga imeendelea kuimarisha mbio zake za kulitetea taji la Ligi Kuu NBC baada ya kuichapa Mashujaa FC bao 1-0 katika mechi ya ligi hiyo iliyopigwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 65 na hivyo kuiacha Azam FC inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi 11 na mahasimu wao Simba walio nafasi ya tatu kwa tofauti ya pointi 15.
Bao pekee lililoitoa kimasomaso Yanga lilipatikana dakika nne kabla ya mapumziko mfungaji akiwa ni Joseph Guede aliyeitumia vizuri pasi ya Mudathir Yahya kuifungia timu yake bao hilo.
Guede mshambuliaji mpya wa Yanga aliyejiunga na timu hiyo katikati ya msimu huu, katika mechi za hivi karibuni ameanza kuonesha ubora wa kuzifumania nyavu akiwa hadi sasa amefikisha mabao matano.
Yanga sasa inahitaji pointi nane ili iweze kufikisha pointi 73 ambazo kimsingi haziwezi kufikiwa na timu yoyote kwenye ligi hiyo inayoshirikisha timu 16 na ambayo inaelekea ukingoni kila timu ikiwa imebakiza wastani wa mechi kati ya tano hadi sita.
Kwa upande wa Mashujaa, matokeo hayo yanawafanya wabaki na pointi zao 23 katika mechi 25 wakiwa nafasi ya 14 na kama wakishindwa kuzitumia vizuri mechi tano zilizobaki wanaweza kushuka daraja na kucheza Ligi ya Championship msimu ujao.
Soka Yanga yawapiga Mashujaa 1-0
Yanga yawapiga Mashujaa 1-0
Read also