Na mwandishi wetu
Baada ya kuchapwa mabao 4-1 na Azam FC jana Ijumaa, kocha mkuu wa Namungo FC, Mwinyi Zahera amesema haumii na matokeo hayo kwani yalisababishwa na makosa ya kibinadamu ya mchezaji mmoja mmoja.
Namungo ilipokea kipigo hicho katika mchezo wa hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho CRDB (FA) uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Zahera alisema timu yake ilikuwa ikicheza vizuri, inafunguka na inafika kwenye lango la wapinzani lakini makosa madogo ya kibinadamu ndio yamewagharimu na yeye hilo halimuumizi sababu timu haikushindwa kupitia mipango yake.
“Nafikiri mpaka dakika ya 20 walikuwa (Azam) wanaongoza mabao matatu, na magoli yenyewe ukiangalia si magoli ya kitimu, ni magoli ya kosa la kibinadamu la mtu mmoja mmoja, na makosa kama hayo yaliyotokea hakuna ambaye anapanga kwamba afanye hivyo kwenye mipango yake na hiyo ndio imetuumiza.
“Ila kingine hata kama tumefungwa lakini ukiangalia timu inacheza, inafunguka tunafika kwenye goli, kwa hiyo siwezi kulaumu wachezaji wangu sana sababu kosa ni la mtu mmoja mmoja, wakati kipa au mabeki wanataka kumtoka mtu wananyang’anywa unafungwa.
“Yale ni makosa ya mtu binafsi, hivyo hainiumizi sana kufungwa sababu kama tungefungwa nne kwa kuzidiwa zaidi kimpira mpaka unakosa cha kufanya hiyo kweli unaonekana huna unachokifanya,” alisema Zahera.
Kwa matokeo hayo, hatua inayofuata ya nusu fainali ya michuano hiyo, Azam itaumana na Coastal Union kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Mei 18 huku Yanga ikitifuana na Ihefu FC Mei 19, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.