Dortmund, Ujerumani
Kwa nini tulikubali Jadon Sancho aende Borussia Dortmund kwa mkopo? Ni swali ambalo huenda linawatatiza mashabiki wa Man United baada ya mchezaji huyo kuwa moto wakati Dortmund ikiichapa PSG bao 1-0.
Ushindi huo uliotokana na bao pekee la Fullkrug dakika ya 36 umetosha kuwaweka Dortmund katika mazingira mazuri ya kufuzu hatua ya fainali ingawa bado wana mtihani wa mechi ya marudiano wiki ijayo mjini Paris.
Katika mechi hiyo iliyopigwa jana Jumatano ushindi huo ulikuwa gumzo la kwanza lakini hapo hapo kuna habari ya Sancho kwa namna alivyoonekana kuwa bora wakati timu yake ya zamani ikihaha kusaka mafanikio.
Man United haimo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na huenda msimu ujao pia ikakosa kushiriki michuano hiyo mikubwa na yenye hadhi ya juu kwa ngazi ya klabu duniani lakini Dortmund sasa inawaza kucheza fainali ya michuano hiyo huku Sancho akiendelea kuwa moto.
Sancho, 24 mara kadhaa alionekana kuwa msumbufu mbele ya mabeki wa PSG, chenga za hapa na pale, pasi za uhakika hali inayozidi kuwatia tamaa mshabiki wa Man United na kuhoji uamuzi wa kukubali mchezaji huyo aende Dortmund kwa mkopo.
Januari mwaka huu Sancho alilazimika kujiunga na Dortmund baada ya kutibuana na kocha wa Man United, Erik ten Hag ambaye alimtuhumu kwa kuzembea mazoezini lakini Sancho hakukubaliana na hoja hiyo.
Katika utata huo mchezaji huyo aliamua kumjibu kocha wake kupitia mitandao ya kijamii akimlaumu kocha huyo kwa ‘kumtoa kafara’ jambo lililomkera Ten Hag na huo ukawa mwanzo wa mshambuliaji huyo kuuzwa kwa mkopo.
Uamuzi huo wa Ten Hag ambao pengine ulikuwa na nia njema ya kuimarisha nidhamu, huenda sasa unawakera mashabiki na kuona kama wamempoteza mtu muhimu ambaye huenda angekuwa msaada wakati huu timu yao inapohaha kusaka mafanikio.
Haishangazi kuona Dortmund sasa wanapiga hesabu za kuhakikisha mshambuliaji huyo anaendelea kuwa na timu hiyo msimu ujao kwa namna ambavyo amekuwa bora na mwenye msaada kwa timu.
Na pengine huenda Sancho akashuhudiwa akicheza mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu dhidi ya Real Madrid au Bayern Munich lakini hiyo ni kama watauvuka mtihani wa PSG.
Kimataifa Sancho awa moto Dortmund
Sancho awa moto Dortmund
Read also