Munich, Ujerumani
Mshambuliaji wa Real Madrid, Vinícius Júnior amempamba kiungo mkongwe wa timu hiyo Toni Kroos (pichani) akisema anajua namna ya kufanya mambo yawe rahisi baada ya kumpa pasi iliyozaa bao la kwanza katika sare ya mabao 2-2 dhidi ya Bayern Munich.
Real Madrid na Bayern ziliumana jana Jumanne katika mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na sasa zinasubiri kurudiana wiki ijayo ili kumpata mshindi atakayecheza mechi ya fainali dhidi ya mshindi kati ya Borussia Dortmund na PSG.
Katika mechi hiyo, Vinicius aliifungia Real Madrid, bao la kwanza dakika ya 24, bao lililotokana na ‘pande’ alilopigiwa na Kroos kabla Bayern hawajasawazisha na kuongeza bao la pili kupitia Leroy Sane na Harry Kane.
Vinicius hata hivyo aliitoa kimasomaso Real Madrid baada ya kufunga bao la pili kwa mkwaju wa penalti na hivyo kufikisha jumla ya mabao matano kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu huu.
Akizungumzia matokeo hayo mara baada ya mechi, Vinicius alielezea mchango wa Kroos ambaye kwa sasa ana miaka 34.
“Toni wakati wote huwa anafanya mambo kuwa rahisi, amenipa zawadi ya bao, kwa pamoja tulifanyia mazoezi kwa sana jambo hili, namjua vizuri Toni naye ananifahamu, nina furaha kufunga mabao mawili na sasa tunahitaji usiku wa maajabu tukiwa nyumbani,” alisema Vinicius.
Kwa upande wake, Kroos naye alitumia nafasi hiyo kumpongeza Vinicius akidai kwamba ndiye aliyetengeneza mazingira ya kupewa pasi hiyo kwa namna alivyofungua uwanja.
“Vini ndiye aliyeniwezesha hadi kutoa pasi, haikuwa pasi ya kipekee lakini ni kutokana na namna alivyojipanga, alifungua uwanja,” alisema Kroos.
Nyota mwingine wa Real Madrid, Rodrygo alisema kwamba pasi aliyoitoa Kroos ilikuwa ya aina yake na kuongeza kwamba umri haujalishi kitu, “Toni wakati wote anakuwa na mbinu hizo, na kiwango ambacho napenda kukiona.