Munich, Ujerumani
Mshambuliaji wa Bayern Munich, Harry Kane amepagawa baada ya jana Jumanne kuweka rekodi ya kuifungia timu hiyo bao la 43 katika mechi ya 43 wakati wakitoka sare ya 2-2 na Real Madrid katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kane, pia amefunga bao lake la 11 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, rekodi ambayo ni nzuri kwa mchezaji wa England na sasa amejawa matumaini akisubiri kwa hamu kubeba taji kubwa barani Ulaya kwa mara ya kwanza.
Msimu huu wa kwanza kwa Kane mambo yangekuwa mazuri zaidi kwake binafsi baada ya kuonesha umahiri wa kuzifumania nyavu lakini tayari timu yake imeshapoteza taji la Ligi Kuu Ujeumani au Bundesliga ambalo limebebwa na Bayer Leverkusen.
Leverkusen wametibua rekodi ya Bayern ambao walikuwa wakiwania kulibeba taji hilo kwa mara ya 12 mfululizo na hivyo rekodi yao sasa inabaki ya kulibeba taji hilo mara 11 mfululizo.
“Msimu huu ni mzuri hadi sasa, kila kitu ambacho tumekuwa tukikipigania mwaka huu katika mashindano kimekuwa kigumu, sasa tunalazimika kwenda kwenye mechi ya marudiano Bernabeu tukiwa kamili wenye kujiamini,” alisema Kane.
“Niko hapa kwa miaka mingi, si mwaka mmoja na mwaka mwingine kuondoka, ni kweli mwanzoni mwa msimu matarajio yalikuwa ni kushinda mataji, Ligi ya Mabingwa ndilo taji kubwa kama tukiliweka taji hilo katika mikono yetu, hakika msimu utakuwa wa kipekee,” alisema Kane.
Sare ya Real Madrid, imempa Kane ambaye pia ni nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya England, imani kwamba Bayern inaweza kufika mbali na kulibeba taji hilo kubwa huku akisisitiza kwamba mechi kubwa kama hizo ndizo zilizomfanya aende Bayern.
“Hizi ni mechi kubwa, mazingira ya kuvutia, hii ndiyo sababu hasa nimekuja hapa, ninataka kucheza mechi hizi kubwa, kuwa katika matukio makubwa,” alisema Kane mshambuliaji wa zamani wa Tottenham.
Mechi ya nusu fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya leo Jumatano
Borussia Dortmund v PSG