Na mwandishi wetu
Kiungo wa Simba, Clatous Chama amefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Sh milioni moja kwa kosa la kumkanyaga makusudi Nickson Kibabage wa Yanga wakati timu hizo zilipokutana Aprili 20, mwaka huu.
Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatano na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kikao cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi cha Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kupitia mwenendo na matukio mbalimbali ya ligi.
Mbali na Chama pia Simba imetozwa faini ya Sh milioni moja huku Yanga ikitozwa faini ya Sh milioni tano kwa makosa ya kuingia kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kupitia milango isiyo rasmi kuelekea katika mchezo huo ulioisha kwa Yanga kushinda mabao 2-1.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa baada ya kuwasili uwanjani, timu hizo hazikutumia mlango rasmi kuingia vyumbani, ikielezwa kuwa Yanga imetenda kosa hilo katika michezo zaidi ya minne.
Imeelezwa kuwa timu hiyo imekuwa ikifanya hivyo katika michezo inayozikutanisha klabu hiyo ndani ya misimu mitatu kuanzia msimu wa 2021-22, 2022-23 na 2023-24 ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kuhusiana na sakata la vyumbani, kamati hiyo inasubiri taarifa ya daktari wa mchezo huo ambaye alichukua sampuli ya hewa kutoka vyumba hivyo viwili kwa ajili ya kuzifanyia uchunguzi.
Inadaiwa kwamba wachezaji wa timu hizo wameshindwa kuingia kwenye vyumba hivyo kutokana na kuwemo kwa harufu isiyo ya kawaida.
Naye, mshambuliaji wa Azam FC, Abdul Selemani ‘Sopu’ ametozwa faini ya Sh 500,000 kwa kosa la kuchukua taulo na maji ya mlinda mlango wa klabu ya Mashujaa FC kisha kuvitupa mbali.
Klabu ya Mashujaa imetozwa faini ya Sh milioni moja kwa kosa la kufanya vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Vitendo hivyo vinadaiwa kufanywa katika mchezo wao huo na Azam FC, wakati wakifanya mazoezi ya mwisho siku moja kabla ya mechi.
Imeainishwa kuwa wachezaji na viongozi wa klabu hiyo walionekana wakimwaga vitu vyenye asili ya unga kwenye viti vya mabenchi ya ufundi na kuweka chupa inayodaiwa kuwa na karatasi nyeupe ndani yake.
Soka Chama afungiwa mechi tatu
Chama afungiwa mechi tatu
Read also