Na mwandishi wetu
Imeelezwa kuwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua ameanza mazoezi rasmi na kikosi cha timu hiyo juzi na anaendelea vizuri kwa ajili ya kurejea kikamilifu kwenye mechi zijazo za timu hiyo.
Hayo yameelezwa Jumatatu hii na ofisa habari wa Yanga, Ali Kamwe akifafanua kuwa maendeleo ya mchezaji huyo raia wa Ivory Coast ambaye aliumia Machi 17, mwaka huu walipoumana na Azam FC katika mechi waliyopoteza kwa mabao 2-1.
“Pacome mpaka sasa tunavyozungumza tayari ameshaanza mazoezi tangu juzi na wenzake, yaani pengine angeweza kulazimisha kucheza mchezo wa Coastal Union lakini tukaona tusiingie kwenye presha ya mashabiki na waandishi kumlazimisha mchezaji arudi wakati kuna kikosi kikubwa,” alisema Kamwe.
Katika hatua nyingine, Kamwe amewaeleza mashabiki wa Yanga kutoona kama kazi imeisha baada ya kuifunga Simba nyumbani na ugenini msimu huu, badala yake waendelee kushikamana na kuipa nguvu timu hiyo mpaka watakapokamilisha mechi za michuano waliyonayo.
Amewataka kuendelea kujitokeza uwanjani kwa wingi na kuipeperusha bendera ya Jangwani kila kona kama ilivyokuwa awali, wakianza na mchezo wao wa Mei Mosi, mwaka huu wa hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho CRDB dhidi ya Tabora United.