Manchester, England
Klabu ya Manchester United inadaiwa ipo tayari kusikiliza ofa kwa mchezaji wao yeyote wa kikosi cha kwanza ikiwa ni moja ya mikakati ya mmiliki mpya wa klabu hiyo, Sir Jim Ratcliffe (pchani) kujenga upya timu yenye uwezo wa kupigania mataji makubwa.
Habari zinadai kwamba mshambuliaji Marcus Rashford naye anatajwa kuwamo katika orodha hiyo hasa baada ya kuonekana dhahiri kwamba hatma yake ipo njia panda ingawa jambo hilo bado halijathibitishwa rasmi.
Rashford, 26, kwa muda mrefu zimekuwapo habari kuwa anatakiwa na klabu ya PSG ya Ufaransa ambayo imewahi kuliweka wazi jambo hilo lakini mchezaji huyo hajawahi kuonesha utayari wowote wa kujiunga na timu hiyo au kukataa.
Wachezaji wengine tegemeo wa kikosi cha kwanza cha kocha Erik ten Hag, Kobbie Maino, Rasmus Hojlund na Alejandro Garnacho, mpango uliopo ni kuhakikisha wanabaki katika timu hiyo.
Wachezaji ambao tayari imeelezwa kuwa majaliwa yao ndani ya kikosi hicho yapo njia panda ni pamoja na kipa Andre Onana, nahodha Bruno Fernandes na beki Diogo Dalot ambaye miezi 12 iliyopita alisaini mkataba mpya wa miaka mitano na timu hiyo.
Habari zaidi zinadai kwamba Ten Hag anatarajia kuwa na kikao kizito na mkurugenzi mpya wa ufundi wa klabu hiyo, Jason Wilcox, kikao ambacho inatarajiwa kitakuja na maamuzi mazito kuhusu mambo ya baadaye ya klabu hiyo.
Wakati yote hayo yakiendelea nafasi ya timu hiyo kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao ni suala jingine linaloendelea kuwatesa vigogo na kujadiliwa kwani kwa sasa Man United ina wakati mgumu kwenye Ligi Kuu England (EPL).
Man United ina mitihani miwili ambayo ikifuzu itaibua matumaini, kwanza ni kuifunga Man City kwenye fainali ya Kombe la FA ili walau ifuzu Europa Ligi lakini pia inatakiwa ifanye vizuri kwenye mechi zilizobaki za EPL ikiwamo ile ya Mei 15 dhidi ya Newcastle.