Abuja, Nigeria
Kocha wa Enyimba, Finidi George ameteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Nigeria ‘Super Eagles’, nafasi ambayo pia ilikuwa ikiwaniwa na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Emmanuel Amunike.
Finidi, nyota wa zamani wa Super Eagles enzi zake za soka la ushindani anakumbukwa zaidi akiwa na klabu ya Ajax ya Uholanzi ambayo mwaka 1995, timu hiyo iliweka rekodi kwa kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa kipindi cha mwaka mmoja na zaidi ya miezi minane, Finidi amekuwa msaidizi wa Jose Peseiro, kocha kutoka Ureno ambaye mkataba wake ulifikia tamati Februari mwaka huu na NFF hawakumpa mkataba mpya.
Super Eagles mapema mwaka huu ilishiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) nchini Ivory Coast na kufikia hatua ya fainali kabla ya kupoteza mbele ya wenyeji waliobeba taji hilo.
Tangu kuondoka kwa Peseiro, Finidi ambaye pia amewahi kuzichezea klabu za Real Betis ya Hispania na Ipswich ya England amekuwa kocha wa muda Super Eagles.
Katika kipindi hicho ameiongoza timu hiyo kwenye mechi mbili za kirafiki dhidi ya Ghana ambayo alishinda kwa 2-1 na dhidi ya Mali ambayo alipoteza kwa kufungwa 2-0.
Taarifa ya mkurugenzi wa mawasiliano wa NFF, Ademola Olajire ilieleza kuwa bodi ya Shirikisho la Soka Nigeria imepitisha mapendekezo ya kamati ya ufundi na maendeleo na kumteua winga wa zamani, Finidi George kuwa kocha mkuu wa timu ya soka ya wanaume ya Super Eagles.
Baada ya kuondoka kwa Peseiro, NFF waliitangaza nafasi hiyo na kupokea maombi mengi kabla ya kuyapunguza majina na kubakiwa na jina la Finidi na mchezaji mwenzake wa zamani Amunike (pichani chini) lakini NFF ikaona Finidi ndiye mtu sahihi.
“Tunajua alikuwa na timu kwa muda mrefu, anaielewa vizuri timu na wachezaji na ingekuwa jambo la hovyo kumpa nafasi mtu mwingine kutoka nje ambaye asingekuwa na muda wa kutosha kuianda timu kwa mechi za kufuzu,” ilieleza taarifa hiyo ya NFF.
Taarifa hiyo pia iliongeza kuwa Finidi amekuwa na Enyimba na amethibitisha uwezo na ni mwenye kuifahamu ligi ya Nigeri kwa mapana hivyo anaweza kuwaona wachezaji wazuri na kuwaita kwenye kikosi cha Super Eagles.
Akiwa mchezaji mahiri na tegemeo wa Super Eagles, Finidi ameichezea timu hiyo mechi 62 kuanzia mwaka 1991 na anajivunia rekodi ya kubeba taji la Afcon mwaka 1994 na bao lake katika sare ya bao 1-1 dhidi ya Algeria ndilo lililoiwezesha Nigeria kufuzu Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza mwaka 1994.
Na ingawa hatma yake katika timu ya Enyimba haijawekwa wazi, kazi ya kwanza ya Finidi ni kuiwezesha Super Eagles kupata ushindi katika mechi mbili za kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Afrika Kusini mjini Abidjan na Benin mjini Uyo.