London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesema timu yake ipo tayari kukabiliana na Man City hadi mwisho katika kulisaka taji la Ligi Kuu England (EPL) lakini akaowaonya wachezaji wake kutobweteka na ushindi wa 3-2 dhidi ya Tottenham Hotspurs.
Arsenal jana Jumapili iliwachapa mahasimu wao wa London, Spurs mabao 3-2 na kuendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa EPL ikiwa imefikisha pointi 80 dhidi ya 79 za Man City.
Ushindi dhidi ya Spurs hata hivyo nusura upotee kwani timu hiyo ilianza kwa kuongoza kwa mabao 3-0 kabla ya Spurs kujibu mapigo kipindi cha pili na kupata mabao mawili.
Arsenal ilineemeka kwa bao la kujifunga la Pierre-Emile Højbjerg na mabao yao mengine mawili yalifungwa na Bukayo Saka na Kai Havert wakati yale ya Spurs yalifungwa na Romero na Son Heung-min aliyefunga kwa penalti.
Arteta aliulizwa baada ya mechi hiyo kama ushindi huo ni ushahidi kuwa wachezaji wake wapo tayari kupambania taji la EPL naye akajibu kwamba hilo ni ukweli asilimia 100 na ameliona hilo tangu mwanzo wa msimu.
“Wananipa sababu ya kuamini hilo kila baada ya siku, tuko katika mwelekeo sahihi, shauku ya kilicho mbele yetu ni nzuri, sote tunatarajia kwamba watapigania hadi mwisho,” alisema Arteta.
Alifafanua kuwa hitimisho huwa linapatikana matokeo yanavyokuwa na iwapo Spurs wangeweza kusawazisha na kuwa 3-3 katika dakika za lala salama hapo kusingekuwa na utayari wa kubeba taji la ligi.
Wakati, Arteta akijipa matumaini, Man City nayo imeendeleza mapambano baada ya kuichapa Nottingham Forest mabao 2-0 na hivyo kuzidi kuisogelea Arsenal kileleni na zaidi ya hilo, timu hiyo imezidiwa mchezo mmoja na Arsenal.
Mabao ya Man City yalifungwa na Josko Gvardiol na mshambuliaji Erling Haaland ambaye amekuwa akiandamwa na majeraha katika siku za hivi karibuni.
Kwa upande wake kocha wa Man City, Pep Guardiola alisema wachezaji wake hawakuwa na presha yoyote katika mechi hiyo licha ya Arsenal kupata ushindi wa 3-2 dhidi ya Spurs.
“Presha inakuwa kwa namna unavyocheza, kama ukicheza vizuri na kutawala mchezo hapo watu watasema hauna presha, na kama ukicheza vibaya watu watasema ni shauri ya presha,” alisema Pep.