Na mwandishi wetu
Baada ya ushindi wa mabao 3-1 jana Alhamisi dhidi ya Yanga Princess, kocha mkuu wa Simba Queens, Juma Mgunda amesema wamefanikiwa kupata ushindi kwa kuwa walitumia muda kuwasoma wapinzani wao wakati mechi inaendelea.
Mgunda alisema alifahamu Yanga wangekuja na mbinu zaidi ya mechi ya awali ya Ligi Kuu ya Wanawake na ndicho kilichotokea, hivyo ili kuwadhibiti ilimbidi asubiri kipindi cha pili ndipo walipofanikiwa kufunga mabao yote matatu kipindi cha pili.
“Tulikuwa tunacheza na timu ambayo tulishacheza nayo kwa hiyo ilikuwa lazima wakija waje na mbinu nyingine tofauti.
“Na kweli waliingia tofauti kwa hiyo tukawa tunawaangalia uzuri wao na upungufu wao na baada ya kipindi cha kwanza tukaelezana cha kufanya mwisho tukashinda,” alisema Mgunda.
Mgunda pia alisema wanajua mechi iliyo mbele yao ni dhidi ya mabingwa watetezi, JKT Queens na ni mchezo mgumu kama ilivyo ligi yenyewe msimu huu.
Alifafanua kwamba kutokana na hilo wanakwenda kujipanga kuhakikisha wanafanya vizuri kiujumla hata kwenye michezo yao mingine iliyosalia msimu huu.
Naye kocha mkuu wa Yanga Princess, Charles Haalubono alisema: “Kwanza nianze kuwapongeza Simba, wamecheza vizuri wametufunga, kuhusu timu yetu naona mabadiliko makubwa ukilinganisha na mechi ya kwanza tulipocheza nao, nafikiri tunahitaji kurekebisha sehemu chache.
Akifafanua zaidi hoja hiyo alisema kwamba wapinzani wao walipata mabao mawili kwa makosa ya ulinzi ingawa ana furaha ya mabadiliko na maendeleo ya kikosi chake mbali na matokeo lakini timu anaiona ikianza kujengeka.