Na mwandishi wetu
Timu za Simba Queens na Yanga Princess zipo tayari kwa mchezo kwa kesho Alhamisi wa ‘derby’ utakaopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam ikiwa ni mwendelezo wa michuano ya Ligi Kuu ya Wanawake.
Wakizungumza leo Jumatano jijini Dar es Salaam makocha wa timu hiyo walisema wanafahamu ushindani uliopo wa ligi baina ya timu hizo na kila mmoja amejinasibu kujipanga vya kutosha kuhakikisha anaibuka na ushindi.
Kocha msaidizi wa Yanga, Fred Mbuna alisema: “Vijana wako salama na wameamka salama na tumefanya maandalizi ya kutosha kama makocha, tumeenda uwanja wa mazoezi tumejaribu kuondoa makosa tuliyokuwa nayo na tumejiandaa kwa ajili ya mchezo.
”Tunafahamu pia ni mechi ya ligi kuu, mechi kubwa, ni mechi ya ‘derby’ hivyo nasi tutaingia kikubwa, tutacheza kikubwa kwa ajili ya kupata matokeo kwenye mchezo huu,” alisema.

Naye, kocha msaidizi wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ alifafanua kuwa wamekuwa na wakati mzuri wakati wa kujiandaa na mechi hiyo na kila mchezaji yuko tayari kupambania jezi ya Wekundu hao.
Mgosi alisema anaamini itakuwa mechi yenye mvuto na ushindani kulingana na malengo ya kila timu ingawa wao wamepania kuwapa furaha mashabiki wao kwa kuibuka na ushindi ili kitimiza malengo yao ya kutwaa ubingwa.
Timu hizo zenye maskani yake Kariakoo, Dar es Salaam zinakutana Simba ikiwa kileleni mwa msimamo kwa pointi 31 ilizokusanya kwenye mechi 11 wakati Yanga iliyocheza mechi 10 ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi 21.
Nafasi ya pili katika ligi hiyo inashikiliwa na mabingwa watetezi, JKT Queens wenye pointi 25 baada ya mechi 11.