London, England
Baada ya kuchapwa mabao 5-0 na Arsenal kwenye Uwanja wa Emirates jana Jumanne, kocha wa Chelsea, Mauricio Pochettino amesema timu yake ni kama iliacha kucheza soka na ilikuwa laini.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu England (EPL), Chelsea ilikwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa bao 1-0 lakini kipindi cha pili ikajikuta ikichapwa mabao manne katika muda usiozidi dakika 18.
Matokeo hayo mabaya kwa Chelsea yameweka rekodi ya kuwa kipigo kikubwa zaidi katika London Derby tangu mwaka 1986.
“Hakuna ugumu wowote wa kuelezea hali ilivyokuwa, kila mmoja aliona, hatukuwa tukipambana tangu mwanzo wa mchezo,” alisema Pochettino.
“Baada ya kufungwa goli la kwanza timu ilikuwa laini, ilinisikitisha tangu tulipoanza kwa sababu tulitakiwa kuwa na nguvu na kupambana vizuri, hatukuonesha ushindani, hatukuwa makini na mazingira ambayo ilikuwa rahisi kuyapatia suluhisho, na hiyo ndiyo sababu hasa iliyonikatisha tamaa,” alisema Pochettino
Katika mechi hiyo, Pochettino alifanya mabadiliko matatu katika safu ya ulinzi akimpumzisha Trevoh Chalobah na Thiago Silva wakati Malo Gusto alikuwa majeruhi baada ya kuumia katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Man City.
Pochettino alisema timu yake ilipambana vizuri katika mechi na Man City ambayo pia walipoteza lakini akashangaa kushindwa kufanya hivyo siku tatu baadaye na kuongeza kuwa huenda timu haikuwa ‘fresh’.
“Tulikuwa tukizungumza wakati wa mapumziko kuhusu kuanza kipindi cha pili katika namna tofauti lakini hatukufanya hivyo, tulipofungwa bao la tatu timu ni kama iliacha kucheza, hali ilikuwa ngumu,” alisema Pochettino.
Kocha huyo hata hivyo alikataa kuzungumzia wachezaji waliokosekana katika mechi hiyo kwa kile alichosema kwamba si haki kuzungumzia jambo hilo kwani tangu mwanzo wa msimu wamekuwa wakiwakosa wachezaji wengi karibu kila baada ya wiki.
Mabao ya Arsenal katika mechi hiyo yalifungwa na Trossard dakika ya nne wakati mengine yalifungwa na White dakika za 52 na 70 na Havertz dakika za 57 na 65.
Kwa ushindi huo Arsenal sasa inashika usukani EPL ikiwa imefikisha pointi 77 katika mechi 34 ikifuatiwa n Liverpool yenye pointi 74 katika mechi 33 wakati Chelsea imeshuka hadi nafasi ya tisa ikiwa na pointi 47 katika mechi 32.