Barcelona, Hispania
Kocha wa Barca, Xavi Hernández ambaye tayari ametangaza nia yake ya kuachana na timu hiyo baada ya msimu huu inadaiwa atakutana na mabosi wake katika kikao chenye lengo la kumshawishi abadili uamuzi huo.
Januari mwaka huu, Xavi alitangaza mpango wake wa kuachana na timu hiyo lakini katika siku za karibuni kumekuwa na habari za ndani zinazodai kwamba kocha huyo anashawishiwa ili afute mpango huo.
Rais wa klabu hiyo, Joan Laporta na wasaidizi wake wa karibu, Rafa Yuste ambaye ni makamu rais na mkurugenzi wa michezo, Deco wote wamewahi kuzungumzia nia yao ya kumtaka Xavi aendelee kuinoa Barca.
Xavi pamoja na kutakiwa abaki katika timu hiyo, mambo yake kimsingi si mazuri kwani Barca huenda ikamaliza msimu bila taji, tayari imetolewa na PSG kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika Ligi Kuu Hispania au La Liga, zikiwa zimebaki mechi sita kabla ya ligi hiyo kufikia tamati, Barca imeachwa na vinara Real Madrid kwa tofuati ya pointi 11.
Habari za ndani zinadai kwamba kikao na kocha huyo kinatarajia kufanyika wiki hii au wiki ijayo huku ikieleweka kwamba mabosi wanataka kuanza maandalizi ya msimu ujao huku wakitaka kujua kama shauku yao ya kutaka kuendelea na kocha huyo itafanikiwa.
Pamoja na ukweli kwamba huu si msimu mzuri kwa klabu hiyo, bado vigogo wanathamini kazi iliyofanywa na Xavi tangu akabidhiwe majukumu mwaka 2021.
Zaidi ya hilo klabu hiyo isingependa kujiingiza katika gharama za kuajiri kocha mwingine kutokana na mazingira magumu ya kifedha yaliyowazunguka kwa mujibu wa kanuni za La Liga.