Na mwandishi wetu
Kocha Msaidizi wa Azam FC, Youssouph Dabo amesema kama wataendelea na kasi waliyonayo sasa bila shaka mwisho wa msimu mashabiki na wadau wa timu hiyo wanaweza kufurahia taji la Ligi Kuu NBC.
Dabo amezungumza hayo baada ya timu yake kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ihefu FC katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yameifanya Azam kufikisha pointi 54 ikijiimarisha katika nafasi ya pili baada ya kucheza mechi 24, wakizidiwa na vinara Yanga wenye pointi 58 katika mechi 22 walizocheza hadi sasa.
“Kuhusu ubingwa baada ya ushindi wa Ihefu, niseme bado mechi sita lakini tulianza kuhesabu pamoja na hii (Ihefu) kwamba bado saba ambazo ni sawa na pointi 21 na sasa tunapaswa kuendelea na kasi tuliyonayo,” alisema.
“Nafikiri wachezaji, makocha, viongozi tunafanya kazi kuhakikisha tunawafurahisha mashabiki na kama tutaendelea hivi basi mwisho wa msimu tutakuwa na furaha,” alisema Dabo raia wa Senegal.
Akiuzungumzia ushindi wao dhidi ya Ihefu, Dabo alisema wamepata ushindi mwembamba kutokana na kutotumia nafasi nyingi walizotengeneza kipindi cha kwanza na kipindi cha pili.
Dabo pia alisema kwmaba walfahamu ubora wa Ihefu na ndio maana walitengeneza uwiano bora wa safu yao ya ushambuliaji na ulinzi katika mchezo huo.
Ihefu ambayo imecheza mechi ya tano ya ligi bila ushindi, kocha wake mkuu, Mecky Maxime alisema: “Kikubwa ligi ndivyo inavyokwenda, unaweza kuingia na mipango yako ya ushindi lakini ukafungwa, ukadroo (sare) au ukashinda kwa hiyo bado hatujakaa sawa.
Maxime alisema kwamba kikubwa kilichowangusha katika mechi dhidi ya Azam ni mawasiliano na pia walichelewa kuwa mchezoni kwenye dakika 10 za awali ndio maana wakaadhibiwa lakini wanaendelea kufanya marekebisho kwa ajili ya mechi zijazo.”