Madrid, Hispania
Kocha wa Barca, Xavi Hernandez na kipa wake Marc-Andre ter Stegen wamelalamikia kukosekana teknolojia ya ‘goal line’ baada ya timu yao kulala kwa mabao 3-2 mbele ya mahasimu wao, Real Madrid jana Jumapili.
Real Madrid walipata ushindi huo kwa bao la dakika za lala salama lililofungwa na Jude Bellingham na kuifanya timu hiyo kuendelea kushika usukani katika La Liga kwa tofauti ya pointi 11 zikiwa zimebaki mechi sita kabla ya kumalizika kwa ligi hiyo.
La Liga ni kati ya ligi ambazo hazijaanza kuitumia teknolojia hiyo jambo ambalo limewakera Barca kutokana na tukio la mpira uliopigwa na Lamine Yamal na kuokolewa na Andriy Lunin wakati huo matokeo yakiwa sare ya 1-1 wakiamini mpira huo ulishavuka mstari.
“Nakosa neno la kuelezea kuhusu kilichotokea kwenye mstari wa goli, inakera sana kwenye soka, pesa zipo nyingi mno kwenye soka lakini hazitumiki kwa mambo muhimu,” alisema Ter Stegen.
Kipa huyo aliongeza kwa kusema kwamba anashindwa kuelewa ni kwa nini haziwezi kuwepo pesa za kuifanyia kazi teknolojia hii ambayo ipo kwenye ligi nyingine.
Kwa upande wake Xavi (pchani juu) aliponda kukosekana kwa teknolojia ya ‘goal line’ nchini Hispania baada ya timu yake kupoteza mechi hiyo maarufu El Classico iliyopigwa kwenye dimba la Santiago Bernabeu.
“Nakubaliana kabisa na Ter Stegen, inakera mno kwa kukosa teknolojia ya ‘goal line’, kama tunataka kusema kuwa hii ni ligi bora duniani, tunahitaji teknolojia hii, kila kitu kilionekana, picha zipo, mtazamo wetu leo ni wa kukosekana haki,” alisema Xavi.
Rais wa La Liga, Javier Tebas aliwahi kujibu madai ya kutokuwapo kwa teknolojia hiyo kwenye ligi hiyo kwa kutolea mifano kwenye nchi ambazo teknolojia hiyo imekuwa na makosa.
Barca waliianza mechi vizuri kwa kupata bao la kwanza mapema dakika ya sita lililofungwa na Andreas Christensen kabla ya Vinicius kusawazisha kwa mkwaju wa penalti.
Barca walifanikiwa kuongeza bao la pili lililofungwa na Fermin Lopez lakini Real Madrid wakajajibu mapigo kwa kusawazisha safari hii kupitia Vazquez na hatimaye Bellingham kukamilisha bao la tatu.