Na mwandishi wetu
Makamu Rais wa Yanga, Arafat Haji amesema kuwa wachezaji wa timu yao wana morali kubwa ya mchezo wao dhidi ya Simba wakiwa na kumbukumbu ya ushindi mnono wa mabao 5-1 katika mchezo wa mwisho baina ya timu hizo.
Haji amezungumza hayo leo Jumatano jijini Dar es Salaam akieleza kuwa pamoja na morali hiyo lakini wanatambua ugumu wa mechi hiyo na wanajua umuhimu wake kwa kuwa ni miongoni mwa mechi zitakazowapa mwanga mzuri kuelekea kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu NBC.
“Hakuna mchezaji anayetaka kucheza mechi ya ‘derby’ halafu hana morali, wachezaji wote wana morali kubwa kulingana na matokeo ya mwisho ya wapinzani tulipokutana nao na kila mmoja anaamini yale matokeo yamepita na sasa tunaenda kuanza upya.
“Na hii ni mechi ambayo itatupa mwanga wa ubingwa maana hii ni mechi muhimu kwetu kuelekea kwenye safari yetu hiyo ya kutetea ubingwa wetu, hivyo tunaitazama vizuri na uzuri wachezaji wanafahamu ni mechi yenye uzito wa namna gani uwanjani,” alisema Haji.
Wababe hao wataumana Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam huku Yanga ikiwa kinara wa ligi hiyo kwa pointi 50 baada ya mechi 21, Simba ikikamata nafasi ya tatu kwa pointi 46 baada ya kushuka dimbani mara 20.