Madrid, Hispania
Kiungo wa Real Madrid, Jude Bellingham amesema VinÃcius Júnior na wachezaji wengine wenye asili ya Afrika wanahitaji kuungwa mkono katika kukabiliana na tatizo kubwa la ubaguzi wa rangi katika soka Hispania.
Bellingham ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya England amesema kwamba udhalilishaji ambao baadhi ya wachezaji wamekuwa wakikumbana nao ni kero kubwa.
Hivi karibuni picha za televisheni zilimuonesha shabiki mmoja akionesha ishara za ubaguzi wa rangi kwa mchezaji wa Real Madrid, Aurelien Tchouaméni baada ya mchezaji huyo kufunga bao pekee katika mechi ya La Liga dhidi Real Mallorca, mechi ambayo Madrid ilitoka na ushindi wa 1-0.
Kwa kipindi kirefu, VinÃcius amekuwa akiandamwa na kadhia za ubaguzi wa rangi kutoka kwa mashabiki wa timu pinzani likiwamo tukio kubwa katika mechi dhidi ya Valencia msimu uliopita, tukio ambalo lililalamikiwa duniani kote.
“Sijui lolote kuhusu tukio la Tchouaméni, katika mechi za La Liga tunazokuwa ugenini, ni kama vile unalazimika kuzoea tukio ambalo hata sikuwa nikilifahamu, tatizo ni kubwa,” alisema Bellingham.
“Nguvu lazima ziongezwe, iwe ni adhabu au namna ya kukabiliana na jambo hili, au ukali katika kukabiliana nalo,” alisema Bellingham.
Mchezaji huyo aliongeza kuwa linakuwa jambo baya kwa mchezaji pale anapojiandaa kwa mechi akijua kwamba atakumbana na kadhia za ubaguzi wa rangi na kuwataka wenye mamlaka kuongeza ukali hasa kwa yale yanayomkuta Vini (Vinicius Jr).
Bellingham ametoa kauli hiyo jana Jumanne wakati leo Jumatano jioni, timu yake itaumana na Man City katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye dimba la Itihad baada ya sare ya mabao 3-3 katika mechi ya kwanza iliyopigwa Bernabeu wiki iliyopita.