Na mwandishi wetu
Uongozi wa Singida Fountain Gate umefunguka kuwa unaendelea na uchunguzi kuhusu utata wa kutoroka kambini kwa kipa wao, Beno Kakolanya.
Wakati uongozi ukichunguza suala hilo zipo habari kwamba kipa huyo aliomba ruhusa huku kukiwa na taarifa za kuhujumu timu katika mchezo wao dhidi ya Yanga waliofungwa mabao 3-0.
Inadaiwa saa chache kabla ya mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Kirumba, Mwanza, Singida FG ilitoa taarifa kwa umma ya kuondoka kambini kwa kipa huyo wa zamani wa Simba na Yanga bila ya ruhusa kutoka kwa uongozi.
“Huu ni utovu wa nidhamu alioufanya Kakolanya maana mtu kuondoka kazini kwako bila ruhusa maana yake huo ni utovu wa nidhamu na utashughulikiwa maana uongozi hautaki mambo hayo na uko makini katika kuhakikisha nidhamu inafuata mkondo wake,” alisema Ofisa Habari wa Singida FG, Hussein Masanza na kuongeza:
“Ni kweli, aliomba ruhusa kwa meneja lakini meneja siye anayetoa ruhusa kama mtu wa mwisho, suala lake lilienda kwa uongozi na uongozi wakasema hapana kutokana na uzito wa mechi na jukumu tulilonalo mbele yetu na walimwambia ataenda baada ya mechi lakini haikuwa hivyo, akatoroka.
“Kwa sasa zipo tuhuma za kuhujumu mechi hii ambayo ni madai na yanaendelea kufanyiwa kazi kupitia kamati yetu ya nidhamu na itakapomalizika tutatoa taarifa zaidi lakini kilichopo ni kwamba lazima hatua za kinidhamu zitachukuliwa katika hili,” alisema Masanza.