Abu Dhabi, UAE
Shirikisho la Soka Saudi Arabia (SAFF) litapitia upya sheria zinazowahusu mashabiki wa soka baada ya tukio la shabiki mmoja kumchapa bakora mshambuliaji wa klabu ya Al Ittihad, Abderrazak Hamdallah.
Katika hafla ya utoaji tuzo baada ya Al Hilal kuichapa Al Ittihad mabao 4-1 kwenye mechi ya fainali ya Saudi Super Cup mjini Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), shabiki mmoja alitoka jukwaani akaingia uwanjani na kumchapa bakora, Hamdallah.
Hamdallah ambaye pia ni mchezaji wa kimataifa wa Morocco baada ya kufanyiwa kitendo hicho, kitu pekee alichofanya ni kummwagia shabiki huyo maji baada ya mzozo baina ya wawili hao.
SAFF kwa kushirikiana na Chama cha Wanasoka Saudi Arabia (PFA) katika taarifa yake ilieleza kushtushwa na tukio hilo la shabiki kumvamia mchezaji wa klabu ya Al Ittihad.
“Kama ilivyo kwa mashirikisho mengine ya soka ya AFC (Asia) na wanachama wengine wa Fifa, kipaumbele cha SAFF ni kulinda usalama na kuhakikisha burudani kwa kila ambaye anapenda kuangalia na kucheza soka,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo pia ilifafanua kuwapo mpango wa kufanya mapitio ya kina kwenye kanuni za usimamizi una lengo la kuhakikisha sheria na kanuni zinawekwa kwa lengo la kutoa adhabu ili kuzuia kujirudia kwa tukio hilo.
“Na ingawa tukio hilo lilitokea nje ya Saudi Arabia, lakini SAFF na PFA tunasimama pamoja katika kipaumbele cha kuhakikisha ustawi wa viwanja vya soka na tutaendelea kutekeleza hatua stahiki ili kuweka mazingira salama kwa kila mmoja anayehusika na soka.”