London, England
Kocha wa Man United, Erik ten Hag amewalaumu wachezaji wake akisema wanapaswa kujua jinsi ya kumaliza mchezo baada ya kushindwa kujilinda na kujikuta wakilala kwa mabao 4-3 mbele ya Chelsea.
Man United katika mechi hiyo iliyopigwa Alhamisi, ilionesha ubora baada ya kufungwa mabao mawili ya mapema, ilipambana na kusawazisha kabla ya kuongeza bao jingine hivyo kuwa mbele kwa mabao 3-2.
Hata hivyo mambo yaliwaharibikia baada ya kujikuta wakifungwa bao la kusawazisha kabla ya kuongezwa bao jingine la nne na hivyo kupoteza pointi tatu ambazo ilionekana dhahiri zilikuwa zao.
“Ilikuwa mechi ya kipekee, ya aina yake ambayo ilijaa ubora,” alisema Ten Hag kuhusu mechi hiyo ya Ligi Kuu England (EPL) huku akiisifia timu yake kwa namna ilivyotawala mchezo.
“Manchester United ilitawala mchezo lakini tukafanya makosa ya mtu mmoja mmoja ambayo yalitugharimu, unapokuwa mchezaji wa Man United unatakiwa kujua namna ya kukabiliana na mazingira ya aina hii,” alisema Ten Hag.
Matokeo hayo yanazidi kuwa pigo kwa mipango ya Man United kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kwani inakuwa imeshindwa kuneemeka baada ya Aston Villa na Tottenham kupoteza michezo yao ya mwisho ya ligi.
“Katika siku tano tumepoteza pointi tano, hili halikubaliki, tulitakiwa lazima tuwe na kiwango cha juu kama tunataka kupambana kwa ajili ya soka la kwenye Ligi ya Mabingwa,” aliongeza Ten Hag.
Baada ya matokeo hayo, Man United itakuwa na mtihani mgumu Jumapili hii kwenye Uwanja wao wa Old Trafford dhidi ya vinara wa ligi hiyo, Liverpool.