Munich, Ujerumani
Kocha wa Bayern Munich, Thomas Tuchel ametangaza rasmi kuitoa timu yake katika mbio za kuliwania taji la Ligi Kuu Ujerumani au Bundesliga msimu huu baada ya kuchapwa mabao 2-0 na Borussia Dortmund.
Bayern ikiwa nyumbani Munich jana Jumamosi ilikumbana na kichapo hicho matokeo ambayo yanaifanya kuwa nyuma ya vinara wa ligi hiyo, Bayern Leverkusen kwa tofauti ya pointi 13.
Leverkusen inayonolewa na kocha Xabi Alonso ambaye ametangaza kuendelea kubaki na timu hiyo licha ya kutakiwa Liverpool, yenyewe ilitoka na ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Hoffenheim.
Alipoulizwa kama Bayern imetoka moja kwa moja katika mbio za kusaka taji hilo, Tuchel ambaye anasubiri msimu huu uishe aondoke katika nafasi hiyo alijibu, ‘ndio, hilo ni dhahiri.
“Baada ya mechi ya leo (jana Jumamosi) hakuna sababu tena ya kuhesabu pointi, ni pointi ngapi kwa sasa, hapana, hongera kwa Leverkusen,” alisema Tuchel.
Kwa Dortmund ushindi huo dhidi ya Bayern unakuwa ni wa kwanza baada ya miaka takriban 10 lakini pia umefufua matumaini ya timu hiyo kumaliza ligi ikiwa kwenye top four.
Alonso sasa anahitaji kuiwezesha Leverkusen kushinda mechi tatu kati ya saba zilizobaki kabla ya kumalizika kwa msimu huu ili timu hiyo itangazwe kinara wa taji la Bundesliga na hivyo kufuta ubabe wa Bayern iliyokuwa ikiwania kulibeba taji hilo kwa mwaka wa 12 mfululizo.
Matokeo ya mechi za Bundesliga Jumamosi…
B Leverkusen 2-1 Hoffenheim
Bayern Munich 0-2 B Dortmund
B Mgladbach 0-3 Freiburg
Frankfurt 0-0 Union Berlin
RB Leipzig 0-0 Mainz
Werder Bremen 0-2 Wolfsburg